STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 10, 2012

Manyika Jr bado aliota pambano la Kongo



KIPA namba moja wa timu ya taifa ya vijana U17 'Serengeti Boys', Peter Manyika 'Casillas' amesema itamchukua muda mrefu kusahau matukio waliyofanyiwa na wenyeji wao Kongo katika pambano lao la marudiano la kuwania kucheza fainali za Afrika.
Manyika, alisema vitisho na fujo walizofanyiwa na wenyeji wao kabla na baada ya kuanza kwa pambano hilo, kwa kiasi kikubwa vilichangia timu yake kupokea kipigo cha mabao 2-0 na kung'olewa mashindano na kuzima ndoto za kufuzu fainali hizo za 2013.
Akizungumza na MICHARAZO katika mahojiano maalum nyumbani kwao, Kigogo jijini Dar es Salaam juzi, Manyika alisema ingawa hilo ndilo pambano lake la kwanza la kimataifa nje ya nchi, lakini hakuwaza kama angekutana na vitimbi kama hivyo ikizingatiwa michuano yenyewe ni ya vijana, pia wenzetu walipokewa vema hapa nchini.
"Kwa kweli niliingiwa na woga na hofu kubwa kwa namna wenyeji wetu walivyotufanyia vituko na fujo ambazo kwa kiasi fulani zilitupotezea umakini uwanjani, licha ya makocha kututia moyo kulipigania taifa," alisema.
Manyika, alisema anadhani kuna haja ya shirikisho la soka Afrika kuyaangalia matukio hayo waliyofanyiwa ikiwemo kupigwa kwa kocha wao msaidizi, Jamhuri Kihwelu 'Julio' ili kuyakemea yasiweze kurudia tena kwani yanaweza kujenga uhasama usio na maana.
Serengeti Boys, walishindwa kurejea rekodi iliyowekwa na wenzao mwaka 2004 walipofuzu fainali hizo za Afrika za U17 kabla ya kuenguliwa kwa kosa la kuchezesha 'kijeba' Nurdin Bakar na nafasi yao kupewa Zimbabwe waliokuwa wamewatoa.

Mwisho

No comments:

Post a Comment