STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, April 5, 2013

Simba kusajili wapya kwa Mil. 300/-

Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala
NYOTA wapya watakaosajiliwa Simba ili kuiongezea nguvu kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wataigharimu klabu hiyo ya 'Wekundu wa Msimbazi' kitita cha takriban Sh. milioni 300, imefahamika.
Taarifa kutoka klabuni kwa vigogo hao wanaoelekea kupoteza taji lao la Ligi Kuu ya Tanzania Bara zilieleza jana kuwa watakaosajiliwa ni nyota watatu wa kigeni na wengine watakaoongezwa watakuwa ni yosso ambao wamekuwa wakiichezea timu yao ya vijana (Simba B) tangu mwaka juzi.
Chanzo kilidai kuwa maamuzi zaidi kuhusiana na suala hilo yalitarajiwa kufanyika katika kikao cha kamati ya utendaji kilichotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam jana jioni.
Imeelezwa kuwa mpango huo wa usajili wa nyota wapya ulijadiliwa katika kikao kingine cha kamati ya utendaji ya klabu hiyo kilichofanyika Jumanne na kuongozwa na mwenyekiti wao, Ismail Aden Rage.
Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alikiri kwamba ni kweli wana mpango wa kukiongezea nguvu kikosi chao kwa kusajili nyota wapya na pia kuongeza yosso wao wanaofanya vizuri. Hata hivyo, Mtawala hakuwa tayari kutaja kiasi cha pesa watakachotumi, ingawa aliongeza kuwa tayari wameanza mikakati ya kusaka fedha za kukamilisha zoezi hilo.
Akieleza zaidi, katibu huyo alisema kuwa usajili wao kwa ajili ya msimu ujao hautawagharimu kiasi kikuwa cha fedha kutokana na malengo yao ya kusajili yosso saba ambao hadi sasa wameshakamilisha mazungumzo yao.
Aliongeza kuwa usajili huo utazingatia ushauri kutoka katika benchi lao la ufundi,  ambalo limeonyesha kuvutiwa na uwezo wa baadhi ya vijana wao ambao wamekuwa wakionyesha kiwango cha juu tangu walipopewa nafasi ya kuanza kikosini katika mechi ya ligi kuu waliyoshinda 2-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

MECHI 5
Katika hatua nyingine, Mtawala alisema kuwa hivi sasa wanajipanga kuhakikisha kuwa wanashinda katika mechi zao tano zilizobaki za ligi kuu ili kulinda heshima yao na kumaliza katika nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo wa ligi baada ya kuona kuwa tayari wameshapoteza nafasi ya kutetea ubingwa wao.
Simba inaendelea na mazoezi jijini Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha wao Mfaransa, Patrick Liewig.  Mechi yao inayofuata watacheza April 13 dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wekundu hao wa Msimbazi wako katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu, wakiwa na pointi 35 wakati watani zao Yanga ndiyo wanaoongoza baada ya kujikusanyia pointi 49, sita zaidi ya Azam wanaowafuatia katika nafasi ya pili na Kagera Sugar wanakamata nafasi ya tatu wakiwa na pointi 37.
 

CHANZO:NIPASHE

No comments:

Post a Comment