STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, October 8, 2013

Cannavaro atamba Yanga kwenda kupata ushindi Kaitaba

Cannavaro (kushoto) akichuana na mchezaji wa Kagera Sugar ligi ya marudiano msimu uliopita
NAHODHA wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ,Yanga Nadir  Haroub 'Cannavaro', amesema licha ya kutambua ugumu wa pambano lao lijalo dhidi ya Kagera Sugar, bado anaamini timu yake itaibuka na ushindi ugenini.
Yanga itasafiri hadi mjini Bukoba, mkoani Kagera kuvaana na Kagera Sugar siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Kaitaba katika moja ya mfululizo wa mechi za Ligi Kuu mwishoni mwa wiki hii.
Mabingwa hao watetezi wanaokamata nafasi ya pili kwa sasa katika msimamo huo, walichezea kichapo cha bao 1-0 katika mechi kama hiyo kwa msimu uliopita iliyochezwa Oktoba 8 na kuwa pambano pekee kupoteza kipindi chote hadi hivi karibuni walipolazwa na Azam katika ligi ya msimu huu.
Cannavaro, beki wa kati wa kutumianiwa wa Yanga anafahamu usumbufu wa wapinzani wao wanapokuwa uwanja wao wa Kaitaba, lakini alisema kwa namna kikosi chao kilichojipanga anaamini wanaenda Kagera kuvuna pointi tatu.
"Tunajua litakuwa pambano gumu na lenye upinzani mkali, lakini Yanga tutapigana kiume ili kushinda kuendeleza wimbi la ushindi tulilolianza," alisema.
Cannavaro anayeichezea pia timu ya taifa, alisema wachezaji wote wa Yanga wana ari kubwa ya kuisaidia timu yao kuendeleza ushindi baada ya awali kuchechemea kwa sare na kupoteza mchezo wao na Azam.
Yanga imepata ushindi mara mbili mfululizo dhidi ya timu za Ruvu Shooting na Mtibwa Sugar na kuwafanya wawasogelee watani zao, Simba wanaoongoza wakiwa na pointi 15, tatu pungufu na ilizonazo Yanga na JKT Ruvu.
Kivumbi cha ligi hiyo kinatarajiwa kuendelea tena kesho kwa michezo minne katika viwanja vinne tofauti ambapo Rhino Rangers itakuwa nyumbani mjini Tabora kuikaribisha Mbeya City kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, huku Oljoro JKT itaialika Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid , Arusha.
Pambano jingine litazikutanisha Azam na Mgambo JKT zitakazoumana kwenye uwanja wa Chamazi na Mtibwa Sugar itakuwa nyumbani Manungu kuikaribisha JKT Ruvu.

No comments:

Post a Comment