STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, July 10, 2010

Shujaa Namba 1 wa Hispania aotae ubingwa





BAO lake lililoizamisha waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia, Carles Puyol, limempa ushujaa wa kipekee katika nchi yake ya Hispania.
Beki huyo anayekipiga Barcelona alijinyakulia ushujaa bila kutegemewa katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ujerumani wa nusufainali ya Kombe la Dunia katikati ya wiki katika timu ambayo imejaa vipaji kama David Villa na Andres Iniesta.
Saa zikiwa zinayoyoma kuelekea muda wa nyongeza katika mechi yenye ushindani mkali, beki huyo mwenye nywele zilizovurugika wakati wote alipiga kichwa cha nguvu kilichoishia nyavuni katika dakika ya 73 na kuwaingiza mabingwa wa Ulaya hao katika mtanange wa kukata na shoka kesho Jumapili dhidi ya Uholanzi.
Lilikuwa bao la tatu la timu ya taifa la mchezaji huyo mwenye miaka 32 aliyekuwa akicheza mechi ya 89 ya kimataifa na liliingiza Hispania fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.
"Puyol 'shark' ametuingiza fainali," mchezaji mwenzake katika klabu ya Barcelona David Villa, ambaye ni mfungaji mwenza anayeongoza katika fainali hizi za Afrika Kusini akiwa na mabao matano, aliwaambia waandishi wa habari akiwa ni mwenye furaha.
Uchezaji wa kuwepo kila mahali wa Puyol katika mchezo huo ulikuwa "maridadi", Villa alisema wakati kiungo Xabi Alonso alisema zaidi: "Tulijenga kambi nje ya eneo lao la hatari kwa dakika kama 10 hivi lakini hatukufunga mpaka Puyol alipochupa kama mkizi na kufunga."
Waziri mkuu wa Hispania Jose Luis Rodriguez Zapatero, ambaye ni shabiki wa Barcelona, alichangia sifa kwa beki huyo, alipoiambia redio ya Hispania: "Si kuruka kule mwanangu, bonge la kichwa cha Puyol! Ni bonge la mchezaji."
Kocha wa Ujerumani Joachim Loew aliiponda timu yake kwa kushindwa kumchunga Puyol aliyeingia kwenye eneo la hatari akikimbia peke yake lakini akasifu "nguvu nyingi" na "kujituma kulikopitiliza" alikoonyesha.

INASTAHILI
Puyol anaamini kuwa 'Furia Roja' imeingia fainali ya Kombe la Dunia kwasababu inastahili na anaisubiri kwa hamu mechi ya kesho Jumapili dhidi ya Uholanzi.
Mabingwa hao wa Ulaya wataikabili 'Oranje' kwenye Uwanja wa Soccer City jijini Johannesburg, na Puyol anajivunia mafanikio ya timu yake mpaka sasa na anadai hakuna anayeweza kusema hawastahili kucheza fainali hiyo.
"Tupo tunapostahili kuwa," Puyol alisema, kwa mujibu wa gazeti la michezo la kila siku la Hispania la Marca. "Timu nzima ina usongo na mechi ijayo na inataka kufanya kitu kikubwa.
"Mechi dhidi ya Uholanzi itakuwa ngumu mno. Ni timu mbili zilizosheheni vipaji na zitakazocheza kufa na kupona kutwaa ubingwa.
"Mechi ya fainali siku zote huwa ni 50/50. Mwanzoni tulikuwa pia tukipewa nafasi kubwa lakini baada ya kufungwa na Uswisi, ikawa balaa."
Alipoulizwa kama mechi ya kesho itakuwa ya mwisho kwake ya kimataifa, Puyol alisema, "Kilichopo mbele ni kitu kizuri sana, baada ya hapo patakuwa na muda wa kufanya tathimini. Sijachukua uamuzi wowote mpaka sasa."

No comments:

Post a Comment