STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 9, 2010

Katibu Mkuu TFF ang'atuka






KATIBU mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, amesema kwamba hataomba kuongeza mkataba mpya wa kuendelea kulitumikia shirikisho hilo baada ya mkataba wake kumalizika mwezi ujao.
Mwakalebela sasa hivi ameelekeza nguvu zake katika kuwania ubunge katika Jimbo la Iringa Mjini, mkoani Iringa kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na blog hii, Mwakalebela alisema kuwa amefikia maamuzi hayo baada ya kulitumikia shirikisho hilo kwa muda wa miaka minne na sasa anataka kuiachia nafasi hiyo kwa mtu mwingine.
Mwakalebela alisema kuwa amepanga kuiandikia barua Kamati ya Utendaji ya TFF kuijulisha maamuzi yake ambayo inatarajia kukutana jijini Dar es Salaam Julai 17 kujadili mambo mbalimbali.
Mwakalebela alisema kuwa akiwa katika nafasi hiyo anajivunia kuona shirikisho linaendeshwa bila ya kuwa na migogoro baina yake na wanachama huku pia ukaguzi wa fedha ukifanyika kila mwaka na kupata cheti chenye alama ya juu.
Alisema pia wadhamini mbalimbali wamejitokeza kuisaidia timu ya taifa, Taifa Stars, na kufanikiwa kushiriki katika fainali za kwanza za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ndani (CHAN).
Aliongeza kwamba anajivunia akiliacha shirikisho hilo likiwa na kituo cha kulea wachezaji wenye vipaji, ambacho tayari matunda ya nyota wake yameanza kuonekana kwa kupata mialiko ya kwenda kufanya majaribio katika klabu za Ulaya na kugombaniwa na klabu kongwe za nchini.
Mwakalebela aliajiriwa katika nafasi hiyo mwaka 2006 baada ya kamati ya utendaji ya shirikisho hilo, kusitisha mkataba wa aliyekuwa katibu mkuu wa kwanza wa kuajiriwa, Ashery Gasabile, kutokana na kushindwa kumudu majukumu aliyopewa.
Wakati huo huo, habari kutoka Dodoma zinasema kuwa, wabunge mbalimbali jana, walimpongeza Mwakalebela kutokana na maamuzi yake ya kujitosa katika kinyang'anyiro cha kuwania ubunge.
Mwakalebela ambaye yuko Dodoma kufuatilia bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, iliyokuwa inawasilishwa jana, walimueleza kwamba waliridhishwa na utendaji wake TFF, nchi imefanikiwa kutangazika kimataifa ambapo ikiwemo kuileta timu ya Brazil.
Walimweleza kuwa wanamtakia mafanikio na watafurahi akirejea katika bunge hilo akiwa kama mbunge kamili na wabunge wengi ni wanamichezo na kwamba muda wote alipokuwa madarakani walifurahishwa na utendaji wake.

mwisho.

No comments:

Post a Comment