STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, July 9, 2010

Wajerumani wataka pweza aliwe hadharani



BERLIN, Ujerumani
BAADHI ya mashabiki wa soka wa Ujerumani wametaka pweza Paul, ambaye amebashiri kiusahihi mechi zote sita za Ujerumani kwenye Kombe la Dunia ikiwemo ya kipigo kinachouma cha nusu fainali kutoka kwa Hispania juzi Jumatano, abanikwe na kuliwa hadharani.
Paul, pweza mwenye umri wa miaka miwili anayeishi katika 'ki-kontena' cha kioo nchini Ujerumani, amegeuka kuwa 'supastaa' wa dunia kutokana na uwezo wake wa kubashiri mshindi wa mechi zote sita za Ujerumani, ikiwemo ya kipigo cha hatua ya makundi walichopata kutoka kwa Serbia na kilichowaondoa kwenye nusu fainali kutoka kwa Hispania.
"Hakuna chakula kitamu kama pweza wa kubanika," alisema Dolores Lusch, shambiki wa Ujerumani anayefanya kazi katika duka la samaki la mjini Berlin. "Mkate katika 'slesi' ndogo nidogo na kisha mbanike kwa kummiminia juisi ya limau, ama mafuta ya olive. Ni mtamu ajabu!"
Wajerumani ambao kwa kawaida hawaamini nguvu za giza wamegeuka kuwa watu wanaoamini sana kuhusu nguzu za utabiri za pweza Paul. Nchi hiyo iliingia ganzi wakati pweza Paul alipoichagua Hispania kuwa ndiyo itakayoshinda mechi dhidi ya Ujerumani baada ya kupatia kuwa itashinda dhidi ya Argentina, England, Ghana na Australia.
Magazeti ya Ujerumani na tovuti yalichapisha mitazamo ya watu kuhusu nini wamfanye pweza Paul, ambapo wengi wamependekeza apikwe na aliwe.
"Mrushe kwenye kikaangio," liliandika gazeti la Berliner Kurier katika kichwa cha habari maarufu kilichoandikwa pia magazeti ya Die Welt, Sueddeutsche Zeitung, The Hamburger Abendblatt na mengineyo.
Utabiri wa pweza Paul umekuwa habari kubwa nchini Ujerumani na kwingineko duniani. Vituo vya televisheni vya Ujerumani vilikatisha ghafla matangazo Jumanne ili kuonyesha 'laivu' tukio la pweza Paul wakati alipokuwa kuwa akitabiri mechi ya nusu fainali ya Kombe la Dunia baina ya Hispania na Ujerumani.
Leo, pweza Paul atatabiri mshindi wa mechi ya Jumamosi baina ya Ujerumani na Uruguay ya kusaka mshindi wa tatu pamoja na mshindi wa mechi ya fainali ya Kombe la Dunia itakayochezwa Jumapili baina ya Hispania na Uholanzi. Vituo vya televisheni vya Ujerumani, Hispania na Uholanzi vinapanga kurusha 'laivu' tukio hilo.
Pweza huyo, ambaye anaaminika kwa baadhi kuwa ndiye kiumbe mwenye akili sana, hupewa fursa ya kuchagua chakula kutoka katika 'vi-kontena' viwili tofauti vilivyotumbukizwa kwenye 'tenki' lake analoishi -- kimoja kikiwa na bendera ya Ujerumani na kingine kikiwa na bendera ya upinzani.
'Ki-kontena' ambacho pweza Paul atakifunua kwanza ndicho huaminika kuwa ndio utabiri wake wa mshindi.
Mvuto uliovikumba vyombo vya habari kuhusu utabiri wa pweza Paul nchini Ujerumani na nje umekuwa mkubwa sana na wachambuzi wameelezea hisia zao kwamba huenda kupatia kwa asilimia 100 kwa utabiri huo huenda kukaingiza imani za kishirikina miongoni mwa wachezaji.
Licha ya mitazamo ya kutaka pweza huyo abanikwe, msemaji wa hifadhi ya viumbe wa baharini ya Sea Life inayomlea pweza huyo, Tanja Munzig, amesema pweza Paul ataendelea kula maisha katika nyumba yake iliyopo mjini Oberhausen, Ujerumani.
"Hakuna lolote baya litakalotokea kwa pweza Paul," alisema mwanamama huyo. "Hakuna mtu anayemuombea baya. Pweza Paul ana rekodi nzuri."
Munzig aliongeza kuwa utabiri wa pweza Paul utaendelea, ambapo leo mchana anatarajiwa kutabiri pambano la fainali za Kombe la Dunia kati ya Spain na Uholanzi litakalofanyika siku ya Jumapili.

No comments:

Post a Comment