STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, August 3, 2010

Chuji, Kaseja warejeshwa Stars





KIPA mahiri wa klabu ya soka ya Simba na kiungo nyota wa Yanga ambao waliondolewa kwenye timu ya taifa na Mbrazil, Marcio Maximo, wamerejeshwa kikosini humo na kocha mpya wa timu hiyo, Mdenmark, Jan Poulsen.
Akizungumza katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu alipowasili nchini Jumamosi usiku kwa ajili ya kurithi mikoba ya kocha Mbrazili Marcio Maximo aliyemaliza muda wake, Poulsen, alisema kuwa alipata taarifa za wachezaji hao na wengine waliowahi kuichezea timu hiyo, lakini ameamua kuwarejesha wawili hao ili kuwapa nafasi ya pili.
"Nimewapa nafasi ya pili ya kuonyesha vipaji vyao, hata kwangu pia, nidhamu ni sehemu ya vigezo vya wachezaji ninaowahitaji, kama watashindwa kuendana na sera zangu nitawaondoa, Boban (Haruna) sijamwita kwa sababu kwa sasa hana timu anayoichezea," alisema kocha huyo.
Mdenmark huyo alisema kwavile yeye ni mgeni na hawafawahamu wachezaji, alianza na wachezaji wa kikosi kilichocheza na timu ya taifa ya Brazili katika mechi ya kirafiki kwa kujua kwamba lazima ndio watakaokuwa wachezaji bora zaidi, kisha akaomba pia majina ya wachezaji wa vikosi vya nyuma na akaulizia kiwango cha kila mmoja hivi sasa na ndipo alipowabaini Kaseja, Chuji na Boban na wengineo.
Alisema wachezaji ambao walikuwepo katika kikosi kilichocheza na Brazil lakini hajawaita, imekuwa hivyo kutokana na kushuka kwa viwango vyao lakini endapo watarejesha viwango vyao atawaita tena huku akianza pia kuangalia vipaji vipya.
Alisema kuwa mipango yake ya muda mfupi ni kuhakikisha Stars inafuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika na kutwaa ubingwa wa Kombe la Chalenji.
Hata hivyo, alisema hajaja na miujiza na kwamba mafanikio hayapatikani mdomoni bali kila mdau kwa nafasi yake kujituma na kutimiza jukumu lake.
"Mafanikio haya yote hayawezi kupatikana kwa maneno, Kenya nao wanasema wanayataka, Uganda pia wanasema hivyo hivyo, lililo muhimu ni wachezaji kujituma, tunatakiwa tushirikiane kuanzia wachezaji, wadhamini, klabu... sio mimi peke yangu nitakayefanikisha," alisema kocha huyo.
Aliitaja mipango yake ya muda mrefu kuwa ni kuendesha mafunzo mbalimbali kwa makocha wa nchini na kusimamia maendeleo ya timu za vijana ambazo ndio msingi wa mafanikio ya nchi zote zilizoendelea katika mchezo huo.
Alisema kuwa wachezaji 27 aliowaita wataripoti kambini leo jioni na kuanza mazoezi kesho kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu ya taifa ya Misri 'The Pharaos' itakayofanyika katika jiji la Cairo Agosti 11.
Kikosi kamili alichokiita ni Kaseja, Jackson Chove, Shabani Kado, Shadrack Nsajigwa, Salum Kanoni, Stephano Mwasika, Juma Jabu, Idrissa Rajab, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kevin Yondani, Aggrey Morris na Erasto Nyoni.
Wachezaji wengine ni Nurdin Bakari, Abdulhalim Humoud, Henry Joseph, Chuji, Nizar Khalfan, Jabir Aziz, Kigi Makasi, Abdi Kassim 'Babi', Uhuru Suleiman, Suleiman Kassim, Mrisho Ngassa, John Bocco, Mussa Hassan 'Mgosi', Jerryson Tegete na Danny Mrwanda.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga, amewataka wadau kumpa ushirikiano kocha huyo mpya na kuongeza kwamba mafanikio hayaji kwa njia ya mkato.
Tenga alisema kuwa kocha huyo atafanya kazi kwa muda wa miaka miwili na akasisitiza kuwa Tanzania haina desturi ya kubadilisha makocha kama nguo.
Alisema pia kwa sasa, kocha huyo atasaidiwa na makocha Juma Pondamali na Syllvester Marsh.
Kaseja alipopigiwa jana alikataa kuzungumzia chochote kuhusiana na maamuzi ya kocha huyo mpya. "Nimesikia taarifa hizo, ila sina chochote cha kusema," alisema.

No comments:

Post a Comment