STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, September 5, 2010

Chagueni CCM Tanzania istawi-Dk Kikwete





MGOMBEA wa Urais wa kiteki ya CCM, Dk Jakaya Kikwete, amewataka wananchi kukichagua chama chake kwa mara nyingine ili kuistawisha nchi, kwa maelezo kwamba vyama vya upinzani vilivyopo ni vya msimu na havina uwezo wa kuongoza.
Dk Kikwete ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano aliyasema hayo leo alipokuwa akiwatuhubia wakazi wa wilaya ya Kilosa katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Wahanga wa Mafuriko lililopo njia panda ya Ilonga na Kimamba, mkoani Morogoro.
Rais Kikwete alisema kuwa, pamoja na kwamba wapinzani wamekuwa wakitoa kejeli dhidi ya utendaji wa CCM, ukweli ni kwamba vyama hivyo havina uwezo wa kuongoza na hivyo ni vema wananchi wakaichagua tena CCM kustawisha maendeleo yaliyopo.
Alisema pamoja na utitiri wa vyama vya upinzani, vingi vyake ni vya msimu tu, ambapo huibuka wakati wa uchaguzi na hasa wanapofanikiwa kuwapata wanaohama toka CCM.
"Wananchi wa Kilosa na Watanzania kwa ujumla nawaombeni muichague CCM kwa mara nyingine kwa kuwa ndio chama pekee bora kinachoweza kustawisha maendeleo ya nchi yaliyopo pamoja na kudumisha amani na utulivu, vyama vingi vya upinzani ni vya msimu tu na hasa vinapofanikiwa kuwanasa wanaohama toka CCM pale wanapogombea na kutochaguliwa," alisema Dk Kikwete.
Dk Kikwete alisema CCM imfanikiwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005 kwa asilimia kubwa katika nyanja na sekta za Afya, Elimu, Maji, Miundo Mbinu, Kilimo na Ufugaji na ikipewa nafasi tena itamalizia sehemu zilizobakia.
Alitoa mfano suala la elimu kwa wilaya ya Kilosa, imefanikiwa kuongeza majengo ya shule kuanzia chekechea hadi sekondari, ambapo alisema kwa mfanoi mwaka 2005 idadi ya wanafunzi katika sekondari ilikuwa ni 6969 ambapo kwa sasa idadi hiyo imefikia 17666 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya wanafunzi 10,000.
Pia alisema juhudi hizo za kuboresha sekta hiyo zinaendana na kuongeza idadi ya walimu ambapop alisema mwaka 2005 idadi ya wahitimu wa ualimu nchi nzima ilikuwa ni 600 tu, lakini awamu ya nne imejitahidi na kufanya idadi hiyo kufikia 16,000.
Alisema, anafahamu idadi hiyo bado haikidhi hivyo serikali yake kupitia CCM inafanya mipango ya kuongeza walimu zaidi kupitia vyuo vyake na vile vya watu binafsi ili kufikia lengo sambamba na kuwezesha kupatikana kwa vitabu, maabara na nyumba za walimu.
Kuhusiana na vitabu,Dk Kikwete alisema tayari jitihada zimeshafanywa kwa kuomba msaada toka kwa nchi marafiki ikiwemo Marekani ambayo imejitolea kutoa jumla ya vitabu 800,000 vya masomo mbalimbali ya sekondari na mapema mwakani itapokea vitabu vingine zaidi ya Mil 2.4.
Alisema hayo na mengine ambayo yamekuwa yakifanywa na CCM tangu iwe madarakani hayawezi kufanywa na vyama vya upinzani na kuwataka wapiga kura kutofanya makosa Oktoba 31 watakapochagua viongozi kwa ajili ya miaka mitano ijayo.
Katika hatua nyingine, mgombea huyo alizungumzia suala la wahanga wa mafuriko yaliyoikumba wilaya hiyo mnamo Desemba mwaka jana, kuwa serikali ipo katika mpango wa kuwajengea nyumba za kudumu wahanga hao wanaishi kambini kwa sasa.
Dk Kikwete alisema kazi ya ujenzi wa nyumba hizo utafanywa na Jeshi la Kujenga Taifa, JKT, kwa lengo la kuwarejesha maisha ya amani na utulivu wakazi hao ambao kwa sasa wanaishi katika nyumba za mabati.
Pia alisema, serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwawa jipya la Kidete pamoja na kujenga tuta jipya la kudhibiti maji ya Mto Mkondoa ambao aliutaja kuwa ndio tatizo lililosababisha mafuriko hayo yaliyoleta maafa makubwa.
Katika ziara yake ya kampeni wilayani humo, mgombea huyo wa CCM alikuwa akisimamishwa yeye na msafara wake na wananchi mbalimbali wa vijiji kwa ajili ya kumueleza kero zao.
Alipofika kata ya Dumila wananchi wa eneo hilo kupitia Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Dumila, Douglas Mwaigumila, walimueleza mgombea huyo juu ya kero zinazowakabili ambapo walizitaja ni huduma ya maji, afya, umeme na uporwaji wa ardhi yao ipatayo ekta 400 shutuma alizozipeleka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya yao.
Dk Kikwete aliwajibu wananchi hao kuwa serikali yao inayatambua kero hizo na tayari ilishaanza kuzitekeleza kwa awamu, huku akishangaa kusikia tukio la uporwaji huyo wa ardhi na kuahidi kulifuatilia.

No comments:

Post a Comment