STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, September 5, 2010

Dk Kikwete akiri watumishi wake wengi ni wezi



MGOMBEA wa Urais wa Chama cha Mapinduzi, CCM, Dk Jakaya Kikwete, amekiri wazi kuwa, watumishi wengi wa Halmashauri ni wezi na ndio wanaokwamisha miradi mingi ya maendeleo.
Aidha mgombea huyo amesema kuwa watanzania wengi wanajitakia kupata maambukizo ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kuendekeza starehe na 'kiherehere' cha kupapia mapenzi yasiyo salama licha ya hamasa mbalimbali zinazotokea juu ya kujikinga na maradhi hayo.
Dk Kikwete aliyasema hayo jana katika mkutano wake wa kuomba kura katika uchaguzi mkuu ujao na kuwanadi wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge wa wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.
Alisema kuwa, pamoja na juhudi za serikali chini ya CCM kutaka kuleta maendeleo kwa wananchi, wapoo baadhi yawatumishi wa Halmashauri ambao ni wezi na wanaoangalia masilahi yao kwa kuzifuja fedha za miradi katika maeneo yao.
"Watumishi wengi wa Halmashauri ni wezi na wanaokwamisha miradi ya maendeleo kwa kuzitumia vibaya fedha wanazopelekewa na serikali kwa ajili ya kuwainua wananchi katika sekta mbalimbali jambo ambalo ni baya," alisema Dk Kikwete.
Katika kukaribia na hilo, mgombea huyo alisema akipata nafasi ya kuchaguliwa tena atahakikisha anapambana nao kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi kama ilivyo kauli mbiu yao kwa kuwa kufanya hivyo kutaondoa kikwazo cha kuwapelekea wananchi maendeleo.
Akizungumza suala la maambukizi ya Ukimwi, mgombea huyo wa CCM, alisema anaamini kuwa, ugonjwa huo unakingika na kuepukika iwapo wananchi wataamua kuzingatia mahubiri na makatazo ya viongozi wa kidini juu ya suala la zinaa.
Dk Kikwete alisema maambukizi mengi yaliyopo nchini ni kama wananchi wanajitakia wenyewe kwa kutawaliwa na kuendekeza starehe na kiherehere cha kukimbilia mapenzi yasiyo salama.
"Kama sio kiherehere ni vipi mwanafunzi badala ya kushughulika na masomo shuleni yeye anakimbilia mapenzi?" alihoji Dk Kikwete.
Alitoa ushauri kwa wananchi juu ya kuwa makini na ugonjwa huo kwa kuoa, kujizuia kuwa waaminifu au kutumia kinga.
Kwani kwa kutokufanya hivyo maambukizi yatazidi kuongezeka na taifa kupoteza nguvu kazi ilihali Tanzania Bila Ukimwi Inawezekana!
Alizungumzia dawa za kurefusha maisha ya waathirika, Dk Kikwete serikali yake inatoa dawa hizo bure na kudai kama kuna wanananchi wanaouziwa basi watakuwa wanaibiwa na wanapaswa kutoa taarifa ili wahusika washuighulikiwe.
Juu ya malaria, aliyodai seikali yake inaumia kuona wananchi wanakufa kwa ugonjwa huo kuliko hata Ukimwi na kudai wameweka mikakati ya kupambana nao kwa kuongeza ugawaji wa vyandarua, kupuliza dawa katika kila nyumba nchi nzima na kuhakikisha wanaua mbu wanaoambukiza ugonjwa huo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment