STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 25, 2011

NYota wa Simba waikamia Mtibwa Sugar J'pili

BAADHI ya nyota wa timu ya Simba, wametamba kuwa wataisambaratisha Mtibwa Sugar watakaoumana nao siku ya Jumapili.
Mabingwa hao watetezi wataikaribisha Mtibwa kwenye uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam katika pambano la mfululizo wa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika mechi yao ya awali iliyochezwa mjini Morogoro na kughubikwa na kashfa ya rushwa, Simba iliisambaratisha Mtibwa kwa bao 1-0.
Pamoja na kutambua ugumu wa pambano hilo, ambalo Mtibwa wameshanadi kutaka kulipiza kisasi na kujiweka kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa ligi hiyo, wachezaji wa Simba wamedai hawatishiki kwa kuamini watashinda.
Juma Jabu 'JJ' beki wa kushoto wa mabingwa hao watetezi, alisema anaamini mechi ya kesho itakuwa na matokeo mazuri kwao kutokana na kiu yao ya kutaka kutetea tena taji lao.
"Hatuna shaka Mtibwa tutawasambatarisha, ili tuweze kutimiza lengo letu la kutetea taji, hivyo wanasimba wasiwe na hofu," alisema Jabu.
Jabu, alisema wanataka kushinda mechi hiyo ili kujiweka vizuri kabla ya kuvaana na watani zao, Yanga Machi 5 kisha kwenda kuvaana na TP Mazembe kwenye mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Naye kiungo mshambuliaji, Rashid Gumbo alijinasibu hana hofu na mechi hiyo ya kesho wala ile ya watani zao, Yanga.
Gumbo, alisema hawawezi kurudia makosa waliyofanya kwenye pambano lao na Toto Afrika ambapo walilazimishwa sare ya 2-2 na hivyo kuitahadharisha Mtibwa ikae chonjo kwa kipigo.
"Wasitarajie mteremko, hatufanyi makosa kama ya Mwanza, tulipolazimishwa sare na Toto," alisema Gumbo mmoja wa wafungaji vinara wa klabu hiyo.
Kama Simba itaifunga Mtibwa ni wazi itarejea kileleni tena ikiiengua Azam, lakini itaombea pia watani zao watakaoshuka dimbani Jumatatu wafanye vibaya ili wasiporomoshwe kwenye msimamo kabla ya kukutana Machi 5.

Mwisho

No comments:

Post a Comment