STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 4, 2012

Simba noma, yabebe mzigo wa matibabu ya akina Boban

UONGOZI wa klabu ya Simba umesema kuwa umechukua jukumu la kuwatibu wachezaji wake Haruna Moshi 'Boban' na Nasoro Masoud 'Cholo' walioumia wakiwa na kikosi cha timu ya taifa 'Taifa Stars' baada ya kukatishwa tamaa na kusuasua kwa shirikisho la soka (TFF) kubeba gharama hizo. Akizungumza jijini Dar, Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema kuwa klabu yake haina muda wa kusubiri matibabu ya TFF kwa wachezaji hao kwasababu ya kuzongwa na kalenda ya mashindano. Simba imeanza maandalizi kwa ajili ya mashindano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati hivyo haiwezi kusubiri mpaka TFF liwatibie 'Boban' na 'Cholo'. Kauli hiyo ya Mtawala imekuja siku moja baada ya katibu mkuu wa TFF, Angetile Osiah, kusema bila kutaja tareeh rasmi kuwa shirikisho litafanya jitihada za kuwatibu wachezaji hao walioumia wakiwa ndani ya kikosi cha Stars. "Sisi ndio tunawalipa mshahara wachezaji hawa, na mtu akigundulika ameumia anatakiwa kutibiwa haraka na hakuna kusubiri," alisema. "Tumeanza kuwatibu ili kocha wetu atakaporudi awakute wachezaji katika hali nzuri na kuendelea na programu zake za mazoezi." Kocha wa timu hiyo Mserbia Milovan Cirkovic atarejea nchini Juni 15, alisema. Kocha huyo ametuma programu ya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya Kombe la Kagame ambayo kwa sasa yanasimamiwa na kocha wa makipa wa timu hiyo James Kisaka. "Timu imeanza maandalizi chini ya Kisaka (James) kwa sababu kocha msaidizi naye ameenda mapumzikoni nchini kwao," alisema zaidi Mtawala. Alisema kocha msaidizi Richard Amatre ataungana na timu Alhamisi baada ya kuwasili nchini Jumatano. Mtawala alisema klabu hiyo imeweka malengo ya kutwaa ubingwa wa Kagame ambao unashikiliwa na watani zao Yanga walioutwaa kwenye mashindano ya mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Simba goli 1-0.

No comments:

Post a Comment