STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, June 4, 2012

Kitale: 'Teja' la kwenye runinga lisiloujua 'unga'

KWA jinsi anavyoigiza na muonekano wake kama 'teja' katika baadhi ya kazi zake za filamu za kawaida na vichekesho, ni vigumu kuamini kuwa msanii Mussa Yusuph 'Kitale Rais wa Mateja' sio mtumiaji wa dawa za kulevya. Mwenyewe anadai hatumii kilevi cha aina yoyote zaidi ya kuigiza tu kama muathirika wa dawa hizo haramu za kulevya. Msanii huyo aliyewahi kutamba na makundi ya Kaole Sanaa na Fukuro Arts Professional, alisema watu wachache wanaoamini kama kweli hatumii kilevi. "Situmii kilevi chochote, sio pombe wala bangi, naigiza tu we mwenyewe unaniona bonge la HB au vipi?" Kitale alisema kwa utani alipohojiawa. Kitale alidokeza chanzo cha yeye kupenda kuigiza kama 'teja' aliyeathiriwa na 'unga' kiasi cha kuwa kibaka ni uzoefu alioupata kwa kuishi karibu na 'mateja'. Kitale, alisema jirani na kwao na sehemu kubwa ya Mwananyamala wapo vijana walioathiriwa na dawa hizo za kulevya, hivyo alikuwa akiwachunguza jinsi wanavyoongea, kutembea na maisha yao kwa ujumla na kujifunza mengi. "We unajua Mwananyamala na maeneo mengi ya uswazi kuna mateja wengi na bahati nzuri karibu na home kuna maskani yao ndio walionisaidia kunifanya niigize kama teja la kutupwa," alisema. Alisema mbali na uigizaji huo kuwa kama 'nembo' yake, lengo lake ni kuishtua jamii jinsi ya kuthibiti tatizo la dawa za kulevya, linaloteketeza kizazi na nguvu kazi ya taifa. "Naigiza hivyo, ili kuizindua jamii na kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, dawa hizi zimekuwa zikiharibu na kupoteza nguvu kazi kwa jinsi zinavyoathiri na kuwa na madhara makubwa kwa taifa letu," alisema. Alisema japo wanaibuka wasanii wanaoigiza kama yeye (Kitale), msanii huyo alidai hana hofu kwa kutambua ataendelea kubaki kuwa Kitale na kamwe hajishughulishi na wasanii hao wanaoiga 'nembo' yake. "Kwa kweli wapo baadhi ya wasanii wameanza kuiga uigizaji wangu, ila sina hofu na wala muda wa kuwajadili, mie naendelea kupiga kazi kwani naamini nitaendelea kubaki kuwa Kitale aliye mmoja tu yaani Rais wa Mateja," alisema. Kitale, aliyeanzia sanaa tangu akiwa kinda wakati akisoma Shule ya Msingi, alisema licha ya umaarufu mkubwa alioupata kwa namna ya uigizaji huo wa kama 'teja' hasa alipong'ara katika tamthilia ya 'Jumba la Dhahabu', alidai wakati mwingine hupata usumbufu. "Ukiacha watu kunishangaa, wapo wengine hudhani uigizaji wangu ni uhalisia wa maisha yangu hivyo huniogopa wakidhani ni teja na kibaka, ingawa huwa naamini ujumbe nilioukusidia umefika kwa jamii," alisema. VIPAJI KIBAO Kitale, mchumba wa Fatuma Salum na baba wa mtoto mwenye umri wa miaka karibu miwili aitwae Ahmed, licha ya kuigiza pia ni mahiri kwa utunzi na utayarishaji wa filamu sambamba na akiimba muziki wa kizazi kipya. Kwa sasa mkali huyo anatamba na wimbo uitwao 'Hili Dude Noma' alioimba na kaka yake Mide Zo na Corner, kikiwa ni kibao cha pili kwake baada ya 'Chuma cha Reli' alichokitoa mwaka jana akiimba na mchekeshaji wenzake, Gondo Msambaa. Msanii huyo alisema kwa sasa anaendelea kumalizia kazi yake ya mwisho kabla ya kuhitimisha albamu itakayokuwa na nyimbo nane akizitaja zilizokamilisha kuwa ni 'Anajifanya Msela' alioimba na Juma Nature, 'Hili Toto' ft. Sharo Milionea na Mide Zo, 'Tulianzishe' na 'Kinaunau'. "Nimebakisha wimbo mmoja tu ambao nimeshautunga na kuufanyia mazoezi ila nasubiri kuafikiana na mmoja wa wasanii nyota nchini ili niurekodi," alisema. Hata hivyo Kitale alikiri kuwa, licha ya umaarufu mkubwa aliopata katika uigizaji, bado haridhiki na masilhai anayopata katika fani hiyo akidai hailipi kama ilivyo kwa muziki. Alisema, uigizaji haulipi kama muziki, lakini bado hana mpango wa kuachana na fani hiyo. "Kwenye uigizaji tunaambulia sifa tu, ila masilahi ni madogo mno tofauti na muziki, hata hivyo siwezi kuachana na fani hii kwani nimeshaizoea, na kwa sasa najiandaa kutoa kazi mpya nikishirikiana na Sharo Milionea," alisema. Alizitaja kazi hizo mpya ni; 'Sharo Madimpoz', 'Sharo Crazy', 'Sharo Taxi Driver' na 'Drug Dealer' wanazoziandaa na msanii mwenzake. Kitale alisema hizo ni baadhi ya filamu walizopanga kuzitoa ndani ya mwaka huu, sambamba na kuendelea na masuala ya muziki akidai kila mmoja imekuwa ikimpa mafanikio makubwa. FILAMU Kitale aliyezaliwa miaka kadhaa iliyopita mjini Morogoro ni shabiki mkubwa wa soka, mchezo aliowahi kucheza utotoni kabla ya kutumbukia kwenye uigizaji, akizitaka timu anazoshabikia kuwa ni Yanga na Manchester City. "Aisee katika soka huniambii kitu, licha ya kulicheza pia ni mnazi mkubwa wa Yanga na naipenda mno Manchester City," alisema. Kitale anayependa kula ugali kwa dagaa na kunywa vinywaji laini, alisema mbali na kucheza 'Jumba la Dhahabu' iliyompa umaarufu mkubwa, ameigiza pia filamu kama 30 na kushiriki kipindi cha vichekesho cha 'Vituko Show'. Alizitaja baadhi ya kazi hizo kuwa ni 'Back from Prisons', 'Mtoto wa Mama', 'Alosto', Mbwembwe', 'More than Lion' aliomshirikisha msanii wa muziki wa kizazi kipya wa kundi la Tip Top Connection, Abdulaziz Chende 'Dogo Janja'. Kitale, anayemzimia King Majuto aliyeigiza naye baadhi ya kazi, alisema fani ya sanaa nchini imepiga hatua kubwa, isipokuwa inakwamishwa na wajanja wachache wanaowanyonya wasanii na kuwafanya wasinufaike na fani hiyo. Alisema ni vema juhudi za kupambana na maharamia ikaongezwa, ili wasanii wa Bongo wanufaike na jasho lao na kuishi kama wasanii wa mataifa mengine ambao ni matajiri kuliko hata watu wa kada zingine. Kitale, anayefurahishwa na tukio la kuzaliwa kwa mwanae, akihuzunishwa na kifo cha mjomba wake aliyekufa kwa ajali ya gari, alisema matarajio yake ni kumuomba Mungu ampe umri mrefu na afya njema afike mbali kisanii. Alisema angependa kujikita zaidi katika muziki na kutoa kazi zake binafsi za filamu ili kunufaika na jasho lake baada ya kutumikia watu wengine bila kunufaika zaidi ya kuambulia sifa tu.

1 comment:

  1. oyaaa nakukubali kinoma mwanaaa kaza hivyo hivyo skufichi siyo mimi tuuu wengi tunakukubali upo juu kitale ktk vibwagizo vyako vinavyoniua ile ya kwa mganga pale unapomalizia "niende mahali pema peponi halaf lile neno aleluya namna unavyolitamka,na ile ya unaulizwa uko wapi na ile mlookota fuko la mavi mkadhani kuna pesa!!thanx bro na enjooy sana sana film zenu na family yangu.khatib issa france,paris,stanligrad

    ReplyDelete