STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 8, 2013

Mtebe aahidi kuendelea kufunga VPL kama Vermelien

Salvatory Venance Mtebe 'shujaa' mpya wa Mtibwa Sugar
 
BEKI mahiri wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar, Salvatory Mtebe ambaye ameibuka kuwa shujaa wa klabu hiyo katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, ameahidi kuendelea kufunga mabao kadri awezavyo ili kuhakikisha Mtibwa inamaliza ligi katika 3 Bora.
Mtebe aliyeitungia Simba wakati Mtibwa ilipopata ushindi wa bao 1-0 kwenye mechi ya marudiano na kurudia tena majuzi mjini Tanga alipofunga bao pekee katika mechi yao dhidi ya Mgambo JKT, alisema anajisikia faraja kuibeba timu yake.
Mchezaji huyo alisema kadri atakavyokuwa akipata nafasi atakuwa akifunga mradi timu yake ije kumaliza msimu wa ligi ikiwa katika nafasi tatu za juu kwa vile ubingwa kwao ni vigumu kutokana na kuachwa mbali na timu za Yanga na Azam.
"Kwa kweli nashukuru kwa kuweza kuifungia timu yao mabao muhimu na kuipa pointi muhimu, nitaendelea kufanya hivyo kila nipatapo nafasi mradi Mtibwa imalize kwenye Tatu Bora. Mashabiki wetu wala wasiwe na hofu na kudhani nabahatisha," alisema.
Mtebe alisema hata kwenye msimu uliopita aliweza kuwa miongoni mwa mabeki waliokuwa na mabao mengi kwa kufunga mabao matatu, hivyo siyo ajabu kuendelea kufanya hivyo msimu huu kwa sababu alishawahi kucheza kama mshambuliaji.
Beki huyo wa kati aliyewahi kuichezea timu ya Atletico ya Burundi, Azam na Kagera Sugar kabla ya kutua Mtibwa misimu mitatu iliyopita, alisema kwa hali ya ushindani uliopo katika ligi ya msimu huu ni vigumu kutabiri bingwa mapema kwa sasa.

No comments:

Post a Comment