STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 8, 2013

IDFA yaipongeza Ashanti kurejea Ligi Kuu, ila yaionya


Bango la Ashanti United walipopanda Ligi Kuu msimu wa 2005-06



Katibu Mkuu wa IDFA, Daud Kanuti (aliyesimama)

CHAMA cha Soka Wilaya ya Ilala, IDFA, kimeipongeza klabu ya Ashanti United kwa kufanikiwa kurejea tena Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini wakiitahadharisha kuwa, inapaswa kuhakikisha wanajipanga vema ili wadumu kuicheza ligi hiyo kwa muda mrefu.
Ashanti ni moja ya klabu mbili zilizopanda ligi kuu msimu ujao nyingine ikiwa ni Mbeya City, baada ya mwishoni mwa wiki iliyopita kupata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Villa Squad na hivyo kujihakikisha uongozi wa kundi lake katika Ligi Daraja la Kwanza, FDL.
Katika Mkuu wa IDFA, Daud Kanuti aliiambia MICHARAZO asubuhi ya leo (Machi 8) kuwa wamefurahishwa na timu hiyo ya Ilala kurejea tena ligi kuu baada ya kusota tangu ilipoteremka msimu wa 2008-2009.
Kanuti, alisema IDFA inaamini kurejea kwa Ashanti katika ligi kuu itaongeza chachu kama ilivyowahi kufanya wakati ikishiriki kwa kuzihenyesha Simba na Yanga kabla ya kupoteza muelekeo na kuteremka daraja.
"IDFA kwa heshima na taadhima tunaipongeza klabu ya Ashanti kwa kututoa kimasomaso wana Ilala kwa kurejea Ligi Kuu, kitu cha muhimu tunaiomba ianze kujipanga mapema ili kuweza kuhimili mikikimikiki ya ligi hiyo msimu ujao," alisema Kanuti.
Kanuti alisema uongozi wa IDFA kama ulivyokuwa begabega kwa klabu hiyo pamoja na wawakilishi wengine wa Ilala katika ligi daraja la kwanza inayoelekea ukingoni ndivyo ambavyo watakuwa pamoja na uongozi wa Ashanti kuhakikisha wanajipanga vema.
Ashanti United ilishawahi kucheza ligi hiyo baada ya kupanda daraja msimu wa 2005 ikiwa pamoja na Kagera Sugar kabla ya kuteremka msimu wa msimu wa 2008-09 ikiwa imewaibua nyota kadhaa wanaoendelea kutamba nchini kama Ally Mustafa 'Barthez',
Juma Nyosso, Juma Jabu, Adam Kingwande,  Mohammed Kijuso na wengineo.

No comments:

Post a Comment