STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 22, 2013

Rais Kikwete azindua Complex ya Azam na kuzipiga 'dongo' Simba, Yanga


 Rais Jakaya Kikwete akizindua rasmi Jiwe la Msingi wa Uwanja wa Azam Complex. (Picha na Habari Mseto Blog)
Rais Jakaya Kikwete akiwa kwenye Uwanja mwingine wa Azam ambao bado upo kwenye matengenezo
 Rais Jakaya Kikwete akikata utepe,wakati wa uzinduzi rasmi wa uwanja wa Azam Complex.
 Rais Jakaya Kikwete akiwapungia mkono  mashabiki wa Azam waliokuja kushuhudia uzinduzi rasmi wa uwanja wa Azam Complex,baada ya kuuzindua rasmi uwanja huo.
 Rais Jakaya Kikwete,akiwa kwenye chumba cha kufanyia mazoezi kwenye Uwanja wa Azam Complex,baada ya kuuzindua rasmi.
 Rais Jakaya Kikwete,akiwa kwenye chumba cha kufanyia mazoezi kwenye Uwanja wa Azam Complex,baada ya kuuzindua rasmi.
Rais Jakaya Kikwete akiwa kwenye Uwanja mwingine wa Azam ambao bado upo kwenye matengenezo.
 
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alipigwa na butwaa baada ya kufika katika makao makuu ya klabu ya Azam yaliyopo Mbande jijini Dar es Salaam jana na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kujenga miundombinu ya kisasa ya timu hiyo.
Rais Kikwete ambaye alikuwa amefuatana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, mkewe Mama Salma Kikwete na viongozi mbalimbali wa serikali, aliweka jiwe la msingi kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa uwanja wa klabu hiyo wa uitwao Azam Complex, kisha akatembezwa kuiona miradi mbalimbali ya wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobaki mwaka huu katika michuano ya klabu ya Afrika.
Akizungumza baada ya kuzindua uwanja huo na kuona utekelezaji wa mipango ya Azam ikiwamo ya kulea vijana wenye vipaji vya soka, rais Kikwete aliupongeza uongozi wa klabu hiyo na kuzipa changamoto klabu kongwe za Simba na Yanga kujifunza kutoka kwao.
Kikwete pia aliipongeza Azam kwa kuwa timu pekee ya Tanzania iliyobakik katika michuano ya kimataifa baada ya Simba na Jamhuri kutolewa katika hatua ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika huku timu hiyo iliyokamata mnafasi ya pili msimu uliopita ikifuzu kwa raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
"Azam wamekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza soka nchini na timu yao sasa ni timu kigogo. Simba na Yanga sasa wanalazimika kujipanga zaidi wanapocheza na timu hii," alisema Kikwete.Akieleza zaidi kuhusu Simba Yanga, rais Kikwete alisema kuwa licha ya kuwa 'mnazi' wa mojawapo miaka iliyopita, klabu hizo zinakabiliwa na matatizo mengi yakiwamo ya tuhuma za ushindi wa kununua, imani za kishirikiana na kukosa viongozi makini.
"Klabu hii (Azam) haina wanachama wengi kama baadhi ya klabu nyingine ambazo wanachama wake wanagombana kila kukicha. Viongozi wa Azam msibweteke kama hawa jamaa kwa kutegemea kamati za ufundi (ushirikina)… hakuna uchawi katika mpira. Kama uchawi ungelikuwa unacheza mpira, Afrika tungelikuwa tumeshatwaa Kombe la Dunia. Ni upuuzi kuwekeza kwenye kamati za ufundi," alisema Kikwete.
"Wapo watu wanawekeza kwenye kusajili wachezaji kila mwaka. Ukifuatilia vizuri, wachezaji wanasajiliwa si kwa sababu wanahitajika, bali wasichukuliwe na timu nyingine, mpira hauko hivyo. Wekeza kwa vijana kwa kuhakikisha wanakula na kulala vizuri. Unakuta kiongozi hajui mchezaji anakula nini na analala wapi.
"Timu hii (Azam) inaendeshwa bila kutegemea wanachama wanaokimbilia kupiga kura kwa kuhongwa. Itakuwa timu kubwa sana, labda mshindwe wenyewe kwa kuamua kutumiwa. Mkikubali kuwa kivuli cha timu yoyote ili kuisaidia, mtashindwa."
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni za Bakhresa (SBB) wanaomiliki Azam, Aboubakar Bakhresa, alimshukuru rais kwa kukubali kushiriki uzinduzi wa uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000.
Alisema imewagharimu Sh. milioni 800 kulinunua eneo walilojenga uwanja huo, ofisi na hosteli za wachezaji na kwamba awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu hiyo tayari imeshawagharimu takriban Sh. bilioni tatu.
Azam ilianzishwa mwaka 2004 ikiwa na muungano wa timu za viwanda vitatu vya SSB. 2005 ilipanda dara la tatu, daraja la pili (2006), la kwanza (2007) na ilitinga Ligi Kuu ya Tanzania Bara 2008.
Hivi sasa, Azam ambayo haijawahi kushuka daraja tangu ipande ligi kuu, inakamata nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ikiwa na pointi 37 baada ya kucheza mechi 19, pointi 11 nyuma ya vinara Yanga walioshuka dimbani mara 20.
Novemba mwaka jana, mshindi mara tatu wa zamani wa tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika, Abedi Pele alipigwa butwaa pia alipofika Mbande na kukiri kuwa amevutiwa mno na jitihada za klabu hiyo katika kukuza soka la vijana.

 

No comments:

Post a Comment