STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 10, 2013

Sunzu, Kazimoto warejesha Msimbazi

Sunzu (kulia)
WAKATI wachezaji Felix Sunzu na Mwinyi Kazimoto wakirejea katika kikosi cha Simba kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kikosi cha timu hiyo kinaingia kambini leo Bamba Beach, Kigamboni.
Sunzu na Kazimoto walitarajiwa jana jioni kuanza mazoezi na wachezaji wenzao kwenye Uwanja wa Kinesi, Sinza jijini na lengo la kuwarejesha baada ya kuomba msamaha ni kukiongezea nguvu kikosi kitakachopambana kuivaa Azam.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema jana kuwa wachezaji wote wataingia kambini leo asubuhi na wanaamini kambi hiyo itawaongezea morali ya kufanya vizuri katika mechi hiyo.
Mtawala alisema kuwa maandalizi  ya mechi hiyo yamekamilika na wachezaji wamepatiwa mahitaji yote muhimu kuelekea mchezo huo muhimu kwa timu yao ambayo imeshapoteza matumaini ya kutwaa ubingwa.
"Kila kitu kinachotakiwa kuandaliwa kimeshafanyiwa kazi na wachezaji wote wanaingia kambini kesho saa nne asubuhi, tunaamini wakiwa huko watapata utulivu na kumsikiliza mwalimu," alisema Mtawala.
Naye daktari wa Simba, Cosmas Kapinga, alisema jana kuwa beki tegemeo wa timu hiyo, Shomary Kapombe, ameshapona na jana jioni alitarajiwa kuanza mazoezi na wenzake.
Kapinga alisema kwamba vipimo vya mwisho vya uchunguzi alivyofanyiwa juzi Jumatatu vimeonyesha kuwa eneo la mfupa kati ya bega na kifua lililokuwa na maumivu limepona.
Simba itashuka dimbani Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Azam walioutapata katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliyofanyika Oktoba 27 mwaka jana.
Mabingwa watetezi Simba ni wa nne katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 35 wakati Azam ambao ni wenyeji wa mechi ya Jumapili wako kwenye nafasi ya pili wakiwa na pointi 43 huku Yanga ndiyo vinara kwa pointi 49.

No comments:

Post a Comment