STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, April 6, 2013

Umony, Tchetche kuongoza mauaji Azam

Nyota wa Azam Humphrey Mieno, Kipre Balou na Brian Umony

WACHEZAJI Salum Aboubakar 'Sure Boy' na Brian Omony leo watakiongezea nguvu kikosi cha Azam dhidi ya Barrack Young Controllers (BYC) ya Liberia kwenye mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho kwa kalbu za Afrika, kwenye Uwanja wa Taifa.
Sure Boy na Mganda Omony hawakuwepo kwenye ushindi wa magoli 2-1 walioupata Azam kwenye mchezo wa kwanza nchini Liberia kutokana na kuwa majeruhi.
Akizungumza na Waandishi wa habari jana, kocha wa Azam, Stewart Hall, alisema kuwepo kwa wachezaji hao kikosini kumempa matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo wa leo.
Alisema kuwa hawana cha kusubiri zaidi ya ushindi dhidi ya wapinzani wao hao.
"Mchezo wa kule Liberia wachezaji Sure Boy na Omony hawakuwepo, lakini mimi kama kocha nimefarijika kuwepo kwao na kesho watakuwepo uwanjani kuhakikisha tunaibuka na ushindi na tunasonga mbele kwenye mashindano haya," alisema Hall.
Viungo hao wawili ni wachezaji wa kutegemewa kwa kiasi kikubwa na Azam ambayo kwa upande wa ligi ya nyumbani inawania kutwaa ubingwa wa kwanza wa Bara katika miaka yake saba tangu kuanzishwa.
Hall alisema pamoja na ushindi kwenye mchezo wa kwanza, hawatabweteka na badala yake watacheza soka la kushambulia zaidi ili kuwapa wakati mgumu wapinzani wao.
Alisema kuwepo kwa Sure Boy katikati huku safu yake ya ushambuliaji ikiwatumia John Bocco na Kipre Tchetche kutaipa Azam ushindi na kuwatupa nje wapinzani wao.
Kwa upande wake, Kocha wa BYC, Robert Lartey Sr, alisema kuwa kwenye mchezo wa leo watacheza soka la kushambulia zaidi kwa kuwa wapo nyuma kwa 2-1.
Alisema kuwa wanaiheshimu Azam FC kwa kuwa ni timu nzuri licha ya kuwa bado changa na kwamba wamejipanga kuhakikisha wanashinda leo japo wanategemea upinzani mkubwa kutoka kwa wapinzani wao hao ambao wanacheza kwenye uwanja wa nyumbani.
Ili kusonga mbele kwa hatua inayofuata, Azam leo ina uwezo wa kufungwa hata si zaidi ya 1-0 ili kuitupa nje ya mashindano timu hiyo inayoongozwa na mtoto wa Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, Robert Alvin Sirleaf ambaye yupo nchini na timu hiyo.
Aidha, Hall aliwataka mashabiki wa soka nchini kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo wa leo utakaoanza saa 10:00 jioni na kuondoa tofauti zao kwa kuwa timu yake inaiwakilisha nchi katika mashindano hayo ya pili kwa ukubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.

No comments:

Post a Comment