STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, May 6, 2013

Zola D naye atangaza kuwania ubunge 2015

Zola D katika pozi
MSANII nyota wa muziki wa Hip hop nchini, Michael Mlope 'Zola D' ametangaza nia yake ya kujitosa kwenye siasa ili awanie Ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Zola D, aliiambia MICHARAZO kuwa, anataka kujitosa kwenye siasa ili kuendeleza harakati zake za kuwazindua na kuwakomboa wananchi kama afanyavyo kwenye fani ya muziki akiwa mmoja wa wanaharakati za kijamii.
Hata hivyo, Zola D ambaye pia ni mwanamasumbwi wa uzito wa juu nchini, hajaweka bayana atawania katika Jimbo gani kupitia chama kipi, licha ya kukiri kwamba atajitosa kwenye mkoa wa Dar es Salaam.
"Natarajia kuwania Ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 katika moja ya majimbo ya jijini Dar es Salaam ila suala la chama na jimbo gani naomba niweke kwanza kwenye mabano mpaka muda muafaka ukifika," alisema Zola D.
Aliongeza kuwa, mpaka sasa vyama vitatu vikuu nchini vimekuwa vikimshawishi kujiunga nao, ingawa alisema chama atakachowani ni kile ambacho kina sera zinazotekelezeka na zitakazowanufaisha wananchi.
"Kiu yangu ni kuona wananchi wanyonge wakipata ukombozi wa kweli wa matatizo waliyonayo, maisha yamekuwa magumu na hakuna wa kuwaonea huruma hivyo nadhani kupitia chama chenye sera zinazotekelezeka naweza kuwasaidia kwani kabla ya kujitosa nimekuwa nikijitolea kwa jamii," alisema.
Kujitangaza kwa Zola D, kumekuja siku chache baada ya msanii mahiri wa filamu, Jacob Stephen 'JB' naye kuweka bayana kuwa atawania ubunge katika moja ya majimboi ya Dar es Salaam akifuata nyayo za Afande Sele aliyeweka bayana tangu mwaka jana na Karapina aliwahi kuwania udiwani Kinondoni.

No comments:

Post a Comment