Rais wa APPT Maendeleo, Peter Kuga Mziray |
Kauli hiyo imetolewa na Rais Mtendaji wa APPT
Maendeleo Peter Kuga Mziray wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii leo
jijini Dar es Salaam.
Mziray alisema tangu rasimu hiyo izinduliwe rasmi
3/6/2013 kumekuwepo na mitazamo mbalimbali ya kuipongeza na kuipinga kwa baadhi
ya watu ambao kimantiki wanaipinga ni
watu wenye malengo yao ya kuwa Marais wa
Tanzania jambo ambalo linaelekea kufa.
Alisema Watanzania hasa wale wa Bara wamekuwa na
kilio cha miaka mingi cha kuhitaji uwepo wa Tanganyika kama ilivyo Zanzibar
lakini hawakusika jambo ambalo kwa sasa limepatiwa muafaka na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Rais Mtendaji alisema mapendekezo ya Tume ni mazuri
kwa asilimia kubwa kwani yamezingatia maoni ya watu wengi ambao walikuwa
wakihitaji rasimu ya katiba iwe hivyo bila kuogopa vivuli vya baadhi ya watu
ambao wamejionyesha dhahiri kutokubaliana nayo.
“Kimsingi naunga mkono mapendekezo ya Tume kwani
yamezingatia mahitaji ya Watanzania wote wa Bara na Visiwani na pia yana nia ya
kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kudumu bila mitafaruku,” alisema.
Alisema wapo watu wameibuka na kusema Serikali tatu
zitakuwa ni kuongeza gharama kubwa kuziendesha jambo ambalo sio kweli kutokana
na ukweli kuwa kila nchi itakuwa ikitumia rasilimali zilizopo katika upande
wake na kuchangia Serikali ya Muungano ambayo haitakuwa kubwa.
Mziray alisema mapendekezo ya Tume yameaanisha mambo
muhimu katika muungano ambayo yapo saba jambo ambalo ni ishara tosha kuwa
hakukuwa na serikali kubwa kama inavyofikiriwa.
Mambo ayalitajwa kuhusika na muungano ni pamoja na
katiba na mamlaka ya jamhuri ya muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama wa
jamhuri ya muungano wa Tanzania, uraia na uahamiaji, sarafu na benki kuu, mambo
ya nje, usajili wa vyama vya siasa na ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo na kodi
yatokanayo na mambo ya muungano.
Aidha alisema rasimu hiyo imeenda mbali pale
ilipoweka wazi kuwa ili mgombea wa Urais atangazwe anapaswa kushinda kura
ambazo zitampatia 50 ya kura zote, pamoja na wagombea wa Urais kupata haki ya
kuenda mahakamani kupinga matokeo.
Rais Mtendaji huyo pia alisema kupunguzwa kwa
madaraka na kuwajibishwa kwa wabunge ambao hawafanyi kazi katika majimbo yao ni
jambo muhimu ambalo Tume inapaswa kupongezwa kutokana na umuhimu wake hasa
ukizingatia kuwa baadhi ya wawakilishi wa wananchi wamekuwa wakiishi mijini
zaidi.
Maziray alisema pamoja na mapendekezo hayo ya tume
ni vema mabaraza ya katiba yakapendekeza adhabu ambazo zinaweza kutolewa kwa
utoro unaofanywa na wabunge jambo ambalo linaweza kurejesha hadhi ya Bunge
ambalo kila siku linaonekana lipo wazi.
Kwa upande mwingine Mziray ameiomba Serikali kuanza
mchakato wa uwepo wa Katiba ya Tanganyika ili iweze kuendana na mchakato wa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jambo ambalo litarahisisha uwepo kwa
serikali hiyo.
Alisema bila kuwepo kwa Katiba ya Tanganyika itakuwa
ngumu kutekeleza mapendekezo ya Tume ambayo yanahitaji kuwepo kwa Serikali tatu
ambazo ni Tanganyika, Zanzibar na Tanzania.
Rais Mtendaji alisema mchakato huo hautakuwa na kazi
ngumu kwani ukweli unaonyesha kuwa maoni mengi ambayo yapo katika rasimu na
yalioachwa yalikuwa yanahusu serikali ya Tanganyika.
No comments:
Post a Comment