SHIRIKISHO la soka (TFF) limesema kuwa baada ya kuundwa kwa kamati ya ligi ambayo ina majukumu ya kusimamia ligi kuu ya Bara, mikataba ya udhamini ya michuano hiyo ya klabu sasa itakuwa ikisainiwa na pande tatu.
Hivi karibuni Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema mikataba ya wadhamini wa ligi kuu Ya Bara itakuwa ikisainiwa na Kamati ya ligi, TFF pamoja na wadhamini husika lengo ikiwa ni kuiboresha ligi na kuepuka manung'uniko kutoka kwa klabu.
"Kwa sasa si TFF peke yake wanaoingia mikataba na wadhamini... mikataba yote ya udhamini wa ligi kuu itakuwa ikisainiwa kwa pamoja na Kamati ya ligi, sisi TFF kama wasimamizi wa mpira hapa nchini pamoja na wadhamini husika," alisema Osiah.
Alisema kuwa hiyo itaongeza ubora wa ligi na kuweka hali ya uwazi wa mikataba ya kudhamini ligi kuu hapa nchini.
Osiah alisema katika mkataba na mdhamini wa sasa wa ligi kuu, kampuni ya huduma za simu ya Vodacom, kuna kipengele kinachotoa nafasi ya kufanya mapitio ya mkataba huo kila msimu unapomalizika.
Alisema kuwa kamati ya ligi imekuwa ikikutana na klabu za ligi kuu na hivikaribuni kamati hiyo itatoa msimamo wake juu ya udhamini wa Vodacom.
Katika msimu uliomalizika hivi karibuni, klabu iliyoshuka daraja ya African Lyon iliingia kwenye msuguano na TFF baada ya kuingia mkataba wa kudhaminiwa na kampuni ya Zantel ambao ni washindani wa kibiashara na Vodacom.
TFF iliiamuru African Lyon kutotumia nembo ya kampuni hiyo ya Zantel kwa kuwa tayari jezi zote za timu za ligi kuu zina nembo ya Vodacom kama mdhamini mkuu wa ligi.
No comments:
Post a Comment