STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, June 1, 2013

Ufaulu Kiadto cha sita waongezeka 'kiduchu'

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEi4wTtUyMRmkPrNtJ_YP5QyVIBrnZSzDWWrb6c0dI3nXm2Ag6H8HZPwgV9fUwi9-b3vStZJ9d9HqAtB_xSOxuQsVeNKt0_09WSNwkBHVUnfO18aXRtSkXP_emGk-F-k1Om3TPSUhYmH_Fl6/s320/DSC_8458.JPG
Wanafunzi wakifanya mitihani
UFAULU wa wahitimu wa Kidato cha Sita mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 0.20 kutoka asilimia 87.65  mwaka jana hadi asilimia 87.85.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk. Charles Msonde kwa niaba ya Katibu Mtendaji,  jumla ya watahiniwa 44,366 sawa na asilimia 87.84 ya waliofanya mtihani wamefaulu.
Alisema kati ya watahiniwa hao, wasichana waliofaulu ni 14,622 na wavulana ni 29,744 sawa na asilimia 87.2.
Akifafanua alisema jumla ya watahiniwa 52,513 waliandikishwa kufanya mtihani huo,  50, 611 sawa na asilimia 96.38 waliufanya huku 1,902 sawa na asilimia 3.62 hawakufanya.
Aliongeza kuwa, watahiniwa wa shule waliofaulu ni 40,242 sawa na asilimia 93.92.
Alisema idadi ya wasichana ni 14,622 na wavulana ni 29,744 sawa na asilimia 87.2 ambapo kwa mwaka jana watahiniwa 40,775 sawa na asilimia 92.30  walifaulu.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea alisema waliofahulu ni 4,124 sawa na asilimia 53.87 wakati kwa mwaka jana walikuwa ni 5,883 sawa na asilimia 64.96 .
UBORA WA UFAULU
Kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule, alisema unaonyesha jumla yao ni 35,880 sawa na asilimia 83.74 wamefaulu katika daraja la 1 -111 wakiwemo wasichana  12,108 sawa na asilimia 87.30 na wavulana 23,772 sawa na asilimia 82.04.
Akifafanua  alisema idadi ya ufaulu daraja la kwanza ni 325 sawa na asilimia 0.76 ambapo wavulana ni 188 sawa na asilimia 0.65 wakati wasichana ni 137 sawa na asilimia 0.99.
Alisema idadi ya ufaulu daraja la pili ni 5,372 sawa na asilimia 12.54 ambapo wavulana ni 3,142 sawa na asilimia 10.84 na wasichana 5,372  sawa na asilimia 12.54.
Katika daraja la tatu jumla ya idadi ni 30,183 sawa na asilimia 70.45 ambapo wavulana 20,442 sawa na asilimia 70.55 na wasichana ni  9,741 sawa na asilimia 70.24.
Alisema katika daraja la nne jumla ya idadi ya watahiniwa ni 4,362 sawa na asilimia 10.18 wavulana ni 3,184 sawa na asilimia 10.99 na wasichana ni 1,178 sawa na asilimia 8.49.
Kwa upande wa daraja sifuri jumla ya idadi ni 2,604 sawa na asilimia 6.08 ambapo wavulana ni 2,021 sawa na asilimia 6.97 na wasichana ni 583 sawa na asilimia 4.20.
MASOMO YALIYOFANYWA VIZURI
Aliyataja kuwa ni Historia, Jiografia, Kiingereza, Kemia, Biolojia, Kilimo, Sayansi ya Kompyuta, Uchumi na Uhasibu ambapo alisema yamefanywa vizuri tofauti na mwaka uliopita.
SHULE KUMI BORA
Alitaja kundi la shule zenye watahiniwa 30 na zaidi na maeneo zilizopo kwenye mabano kuwa ni  Marian girls (Pwani),  Mzumbe (Morogoro), Fedha Boys Dar es Salaam), Ilboru (Arusha), Kisimiri Arusha), St Mary Mazinde Juu (Tanga), Tabora Girls (Tabora), Igowele (Iringa), Kibaha (Pwani) na Kifungilo Girls (Tanga).
SHULE KUMI ZA MWISHO
Alizitaja kuwa ni Osward Mang’ombe (Mara), Green Acres (Dar es Salaam), Bariadi (Simiyu),
Pemba Ismail College (Pemba), Mazizini, High View International, Mwanakwerekwe, Hamamni, Dunga na Lumumba  zote za Unguja.
Akitaja shule kumi zenye watahiniwa chini ya 30 kuwa ni Palloti Girls (Singida), Itamba (Njombe), Kibara (Mara), St. Luise Mbinga Girls (Ruvuma) St. Peter Seminari (Morogoro), Peramiho Girls (Ruvuma), St. James Seminari, Masama Girls, Parane na Sangiti zote za Kilimanjaro).
SHULE ZA MWISHO
Alizitaja kuwa ni St. Mary’s na Mzizima za Dar es Salaam, Mbarali Preparatory, Philter Federal, Mpapa Al-Falaah Muslim zote za Unguja, Hijra Seminari (Dodoma),  Tweyambe (Kagera), Presbyterian Seminari   (Morogoro) Nianjema (Pwani).

TANO BORA KITAIFA
Naibu  huyo alitaja watainiwa watano bora kitaifa katika masomo ya Sayansi kuwa ni Erasmi Inyase (Ilboro Arusha), Maige Majuto (Kisimiri Arusha), Gasper Mung’ong’o (Fedha Boys Dar es Salaam), Gasper Setus (St. James Seminari Kilimanjaro) na Lucylight Mallya (Marian Girls Pwani).
 Pia alitaja wasichana watano bora kitaifa kwa masomo ya Sayansi  kuwa ni Mallya , Edna Kibango (Msalato Dodoma), Sarah Kimario (St. Mary’s Mzinde Juu Tanga), Veronica Mwamfupe (Marian Girls Pwani) na Beatrice Issara (St Marys Goreti Kilimanjaro).
Kwa upande wa wavulana ni Inyase, Majuto , Mung’ong’o, Setus na  Christopher Stanslaus (Mzumbe Morogoro).
Alitaja watahiniwa watano bora kitaifa kwa masomo ya biashara ni Eric Mulogo (Tusiime Dar es Salaam), Alicia Filbert (Nganza Mwanza), Evart Edward  (Kibaha Pwani), Annastazia Renatus (Tambaza) na Peterson Meena  (Mbezi Beach).
Wasichana ni Alicia, Anastazia, Mary Bujiku (St. Anthony’s), Getruda Patrick (Barbor-Johansson (Dar es Salaam) Leticia Kayange (Weruweru Kilimanjaro).

Wavulana ni Mulogo, Edward, Meena, Frank Bunuma (Kibaha Pwani) na Abdallah Juma (Kazima Tabora).
 Watahiniwa watano bora kitaifa kwa masomo ya lugha na Sayansi ya jamii ni Asia Mtini (Barbro-Johansson (Dar), Godlove Ngowo (Majengo Kilimanjaro), Johnason Macha (Njombe), Hamis Mwita Ilboru, Sia Sandi (Marian Girls Pwani).
Alitaja wasichana watano bora katika masomo hayo kuwa ni Aisa, Sia, Jacqueline Agrippa (Masama Girls (Korogwe), Dhulfa Kangungu (Korogwe Girls) na Angelika Chengula (Msalato).
Kwa upande wa wavulana ni Ngowo, Macha,  Mwita, Abubakar Msangule  (Swilla Mbeya) na Alex Mkunda (Kibiti Pwani).

YALIYOZUIWA

Alisema baraza limeyazuia matokeo ya watahiniwa 89 wa shule ambazo hawajalipa ada ya mitihani na kwamba yatatolewa pindi wahusika watakapolipa ada na faini.
Alisema wapo watahiniwa kumi waliopata tatizo la kiafya na kufanya baadhi ya mitihani na wengine 17 walishindwa kufanya mitihani yote kutokana na tatizo hilo ambao watapata fursa ya kuifanya ile ya 2014.
UDANGANYIFU
Alisema wamefuta matokeo yote ya mtihani wa mtahiniwa mmoja wa shule na watahiniwa watatu wa kujitegemea baada ya kubainika kufanya udanganyifu.
Alisema jitihada za serikali katika kukabiliana na tatizo la udanganyifu zimefanya tatizo hilo kupungua kutoka wanafunzi sita mwaka jana na kufikia wanne mwaka huu.
Katika mtihani wa mwaka huu watahiniwa wa shule  43,231 waliosajiliwa, 42,952 sawa na asilimia 99.35 walifanya ambapo wasichana ni 13,883 sawa na asilimia 99.54 na wavulana ni 29,069 sawa na asilimia 99.27.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea kati ya 9,282 waliosajiliwa, 7,659 sawa na asilimia 82.51 walifanya mtihani na watahiniwa 1,623 sawa na asilimia 17.49 hawakufanya.

No comments:

Post a Comment