Kocha wa Liverpool |
KOCHA wa Liverpool, Brendan Rodgers amemweleza mshambuliaji Luis Suarez kwamba ni lazima aombe radhi kwa kutaka kulazimisha kuihama klabu hiyo.
Suarez (26) amekuwa akifanya mazoezi peke yake baada ya kutaka kulazimisha kuhama Anfield katika kipindi hiki cha usajili.
"Kwanza anapaswa kuomba radhi kwa wachezaji wenzake na klabu," alisema Rodgers alipoulizwa kwamba nini kinachofuata anachopaswa kufanya mshambuliaji huyo.
Ofa mbili za Arsenal zikimekataliwa na Liverpool kwa ajili ya mshambuliaji huyo wa Uruguay.
"Nimemuona kwa muda. Najua huyu si Luis Suarez tunayemfahamu na ni kazi yangu kuwalinda mashabiki na wachezaji kwa sababu wanastahili zaidi ya hilo," aliongeza Rodgers.
Kocha huyo wa Liverpool alikuwa akizungumza baada ya timu yake kula kipigo, bila ya Suarez, cha goli 1-0 dhidi ya Celtic katika mechi yao ya mwisho ya ya kirafiki ya kujiandaa na msimu juzi.
"Amekuwa kwa siku kadhaa akifanya mazoezi peke yake," alisema Rodgers, ambaye atamkosa Suarez wiki hii kwa vile anasafiri na timu yake ya taifa ya Uruguay kwenda kucheza mechi ya kirafiki nchini Japan wiki hii.
"Atakaporejea kutoka katika mechi ya kimataifa tunamuangalia kuanzia hapo."
Pigo la karibuni zaidi katika matumaini ya Suarez' ya kuondoka Anfield lilikuja siku moja tu baada ya Rodgers kumtaka akubali kwamba hatauzwa, pale mmiliki wa Liverpool, John Henry aliposema kwamba nyota huyo hatauzwa kwa pesa yoyote kwa klabu yoyote hata nje ya Uingereza.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, ameendelea kusema kwamba bado wanamhitaji mchezaji huyo huku ripoti zikisema kwamba klabu hiyo ya London inapanga kumfanya Suarez kuwa ndiye mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi klabuni hapo kwa kumpa mshahara wa paundi 160,000 kwa wiki endapo atajiunga nao.
(Sunday Mirror)
No comments:
Post a Comment