WAKALA wa Huduma ya Misitu Tanzania umesema katika kutekeleza mpango wa matokeo makubwa sasa (Big Result Now) pamoja na sera ya misitu umefanya maboresho baadhii ili kuongeza mapato Serikali.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Valentino Msusa wakati akiongea na mwandishi wa habari hii leo jijini Dar es Salaam.
Alisema maeneo yaliofanyiwa maboresho ni pamoja na kufanya mapitio ya bei ya mazao ya misitu, kufanya mapito ya mwongozo wa uvunaji endelevu wa misitu wa mwaka 2007, uuzaji wa miti ya misaji (Teak) kwa njia ya mnada na kuimarisha ulinzi katika vizuia na kusitisha ukusanyaji wa maduhuli katika vizuia hivyo.
Msusa alisema kuanzia tarehe 14 Septemba mwaka huu ukusanyaji wa tozo, faini na malipo yoyote ya fedha kwenye vizuia utakuwa umezuiwa ambapo mazao yoyote ambayo yatakutwa sio halali au nnyaraka zake zina mapungufu gari litazuiwa katika kizuia husika.
Mkurugenzi huyo wa Mipango na Matumizi alisema mhusika ambaye atakutwa atapaswa kulipa faini katika vituo vilivyoteuliwa kufanya kazi hiyo na mazao yaliozidi au kutokuwa na nyaraka halali yatateremshwa na kutaifishwa.
“Tumejipanga kikamilifu ili kuhakikisha kauli mbiu ya matokeo makubwa inatokea kutokana na rasilimali zetu ambazo zipo chini ya wakala hii,” alisema.
Msusa alisema katika mapitio ya bei ya mazao ya misitu bei za mazao ya misitu zitapandishwa kwa kuzingatia utafiti uliofanywa na mshauri mwezeshaji ambaye amezingatia gharama za uzalishaji wa miche ya miti hadi kufikia hatua ua kuvunwa.
Kupanda kwa gharama za huduma za vifaa vya uzalishaji na kiwango cha ubadilishaji wa fedha  ya Tanzania na kupanda kwa gharama za vibarua na wafanyabiashara wanaotoa huduma katika mashamba ya miti.
Aidha alisema katika kufanya mapitio ya mwongozo wa uvunaji endelevu wa misitu wa mwaka 2007 maeneo yaliyoboreshwa ni pamoja na kuunda miongozo miwili tofauti iliyotayarishwa kwa ajili ya masahamba ya miti na misitu ya mikoko na ule wa misitu ya asili.
Pia Mkurugenzi huyo alisema pia ni kuboresha takwimu za hali ya misitu hapa nchini na kuweka masharti ya viwanda vya kuchakata mazao ya misitu kama ilivyoanishwa katika sheria ya misitu ya mwaka 2012.
Kwa upande mwingine Msusa alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirkiano na wakala huo ili kuhakikisha jitihada za kukabiliana na uvunaji haramu unapata mafanikio kwa maslahi ya nchi
Alisema wakala huo utaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kutumia vyombo vya habari mbalimbali ili kuhakikisha kuwa elimu juu ya mazao ya misitu inamfikia kila mtu.