Mbunge Ndungulile |
Na Suleiman Msuya
WAKATI ikiwa ni siku chache baada ya Mbunge wa Jimbo
la Kigamboni Dk. Faustine Ndungulile kutoa kauli ya kuita Kamati halali ya
kufuatilia madai ya waathirika wa mabomu ya Mbagala Jijini Dar es Salaam ni
matapeli, kamati hiyo imemtaka aachane na masuala hayo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo
Steven Gimonge wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
Salaam.
Alisema ni vema Mbunge huyo akabainisha kuwa
ametumwa na nani ili kuondoa sintofahamu kwa waathirika kwani wanavyofahamu
suala hilo lipo chini ya maamuzi ya Rais kwa sasa.
Gimonge alisema katika mazingira ya kusikitisha
Mbunge huyo amekuwa akiombwa kuhudhuria vikao ambavyo vinahusisha waathirika
lakini amekuwa hatokeo jambo ambalo ni la kusikitisha.
“Tunapenda kutumia nafasi hii kuelezea sakata la
Mbagala kwani tunaona hali inaanza kuchafuliwa na baadhi ya watu jambo ambalo
hatujui limetokea wapi kwani suala hilo lipo chini ya Rais,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kamati hiyo inamlaani Mbunge
huyo kwa kauli yake hiyo kwani inaweza kuchochea uvunjifu wa amani kati ya
waathirka na Serikali.
Aidha Gimonge alitoa wito kwa wanasiasa kutotumia
majukwaa ya kisiasa kutaka kupoteza haki za wananchi ambao wakuwa wakidai haki
zao kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment