STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 17, 2014

AIBU! Wanawake wawili wanaswa na bangi Arusha

GEDSC DIGITAL CAMERA
Mkuu wa kitengo cha kuzuia na kupambana na madawa ya kulevya Mkoa wa Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Aben Mgode akiwaonyesha waandishi wa habari misokoto 5000 pamoja na baadhi ya magunia 16 ya madawa ya kulevya aina ya bangi yaliyokamatwa kutokana na misako mbalimbali iliyofanyika mkoani hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi Arusha)
****
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
WATU saba wakiwemo wanawake wawili wamekamatwa na misokoto 5000 ya madawa ya kulevya aina ya bangi pamoja na mirungi kilo 47. Tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki iliyopita katika eneo la Mti mmoja lililopo wilaya ya Monduli.
Mafanikio hayo yalitokana na msako shtukizi uliofanywa na jeshi la polisi Mkoani hapa kuanzia saa 12:00 asubuhi mpaka saa 10:00 jioni baada ya kufanya upekuzi katika magari mbalimbali na kupata madawa hayo ambayo yalikuwa yanasafirishwa na watuhumiwa hao kupitia magari ya abiria yaliyokuwa yakielekea Manyara, Singida, Dodoma na Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas watuhumiwa hao walikuwa wanayahifadhi madawa hayo kwenye mifuko ya “plastic” ili yasitoe harufu na kisha kuweka kwenye mabegi.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Godwina Munisi (31) Mkazi wa Sombetini , Mwajuma Kingu (48) Mkazi wa Mbauda,  Fidelis Joseph (48) Mkazi wa Ngarenaro, Selemani Ally (34) Mkazi wa Olmatejoo, Omari Ally (25) Mkazi wa Babati Mkoani Manyara Kasimu Ayubu (39) Mkazi wa Tarakea Rombo Mkoani Kilimanjaro na Yasini Talian (40) Mkazi wa Ngarenaro.
Kamanda Sabas alisema kwamba watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Wakati huo huo katika msako unaoendelea wilayani Longido, jumla ya magunia 16 ya madawa ya kulevya aina ya bangi yamepatikana katika eneo la kijiji cha Leboo baada ya askari Polisi kufanya msako na kufanikiwa kupata magunia hayo 16 yaliyokuwa yanasafirishwa .
Kamanda Sabas alisema kwamba, askari hao walikuwa wanafanya msako usiku na mara baada ya watuhumiwa hao kugundua kuwa wanafuatiliwa walitelekeza magunia hayo 16 na kukimbia. Inasemekana kwamba watuhumiwa hao walikuwa wanatumia wanyama aina ya Punda kusafirishia madawa hayo ambapo magunia yalikuwa yamefungwa mawili mawili.
Hata hivyo Jeshi la Polisi Mkoani hapa bado linaendelea kuwatafuta watuhumiwa hao ili wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

No comments:

Post a Comment