STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, January 17, 2014

Huyu ndiye Amri Kiemba; Kiungo asiyechuja Msimbazi

Amri Kiemba akipowatungua Yanga na kutega sikio kusikiliza kelele za mashabiki wa Msimbazi
WAPO wanaoamini kadri umri wa makipa unavyozidi kusonga mbele ndivyo wanavyozidi kuwa mahiri langoni, tofauti na wachezaji wa nafasi nyingine hasa ya kiungo, beki au ushambuliaji.
Hata hivyo, kwa kiungo mshambuliaji Amri Kiemba, ni tofauti, kwani ujuzi wake wa kucheza na mpira na kufumania nyavu unazidi kuongezeka kadri siku zinavyozidi kusonga mbele na kushangaza mashabiki wa soka.
Msimu mmoja uliopita, kiungo huyo alikuwa akionekana siyo lolote ndani ya Simba kiasi cha kufungashiwa virago na kutakiwa kwenda kwa mkopo katika timu ya Polisi Dodoma iliyokuwa ikichechemea katika ligi msimu wa 2011/12.
Hata hivyo, mchezaji huyo akijiamini bado analiweza soka aliamua kuchomoa kwenda Polisi na kukubali kukaa nyumbani kabla ya kurejeshwa tena Msimbazi msimu uliopita na kuonyesha kiwango kikubwa kiasi cha kuwa 'lulu' ndani ya timu ya Taifa, Taifa Stars.
Katika msimu huo uliopita, Kiemba pia alikuwa gumzo kubwa ndani ya Simba, iliyokuwa imemuona amekwisha kwa kuifungia mabao muhimu na kuziba vilivyo pengo lililokuwa limeachwa na nyota wa Kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya DR Congo, Patrick Mafisango aliyefariki kwa ajali ya gari.
Kasi yake uwanjani, akili ya kuwatoka mabeki na kufumua mashuti makali yaliyolenga lango la mpinzani na kuipa ushidi Simba na Taifa Stars, ilimfanya Kiemba anyakue tuzo ya Mwanasoka Bora kwa msimu wa 2012/13.
Tuzo hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA) ilikuwa kama faraja kwa mchezaji huyo mpole na mcha Mungu kwa jinsi ilivyomfuta machozi kutoka kwenye misukosuko klabuni kwake.
Msimu huu pia mchezaji huyo ameendelea kuonyesha ni moto wa kuotea mbali akiisaidia timu yake kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara duru la kwanza na hata sasa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyotarajiwa kumalizika jana.
Mabao yake mawili, moja dhidi ya AFC Leopards na jingine dhidi ya KMKM yaliisaidia kuivusha Simba hatua ya Robo Fainali kutoka Kundi B kabla ya kufunga jingine na kutengeneza jingine lililoipeleka Wekundu wa Msimbazi kucheza fainali na kulala bao 1-0 kwa KCCA.
Amri Kiemba (kulia) akiitumikia timu ya taifa, Taifa Stars
MKALI
Kiemba aliyewahi kung'ara na Klabu za Kagera Sugar, Moro United, Yanga na Miembeni, licha ya kwamba hana makeke, lakini ni mkali na anayejua majukumu yake uwanjani.
Ingawa amekuwa mkimya na asiyependa kuzungumza na vyombo vya habari, Kiemba anasema siri ya mafanikio yake ni kujituma, kusikiliza makocha na kushirikiana na wenzake mbali na kumtegemea Mungu kwa kila kitu.
Kiemba anayependa kula wali kwa marahage na vinywaji visivyo na kileo, anasema japo amekuwa hapendi kufichua mambo yake hadharani, lakini anashukuru soka kumsaidia kwa mengi na kumuomba Mungu amzidishie umri na kipaji chake aendelee kusakata kandanda.
Nyota huyo, aliyewahi kuzichezea kwa nyakati tofauti timu za taifa kuanzia za vijana U-17 na U-20 kabla ya kuitwa timu ya wakubwa anayoichezea mpaka sasa, anaseme hakuna mechi ngumu aliyowahi kuicheza au kukutana nayo kama ile ya Yanga dhidi ya Esperance ya Tunisia waliposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Anasema anaikumbukwa kwa jinsi wapinzani wao walivyowafunika na ugenini kuwazabua mabao 3-0 kabla ya kutoshana nao nguvu ya kufungana bao 1-1 nyumbani na kung'olewa mashindanoni mwaka 2007.
Kiemba aliyekuwa akicheza soka kama beki wa kati, anasema licha ya kufunga mabao mengi, bao tamu kwake ni lile alililoifungia Kagera Sugar 2004 dhidi ya Polisi iliyosaidia timu yao kupanda Ligi Kuu.
"Nalikumbuka bao lile kwa jinsi nilivyolifunga kiufundi, mbali na kuisaidia kuipandisha Kagera Ligi Kuu msimu wa 2005/2006 tulipowafunga Polisi mabao 3-0," anasema.
Mkali huyo anayependa kutumia muda wake mwingi kusikiliza taarifa mbalimbali za habari kupitia redio na kufanya ibada, anasema soka la Tanzania bado linahitaji mabadiliko makubwa kuweza kufikia kwenye kilele cha mafanikio kwa kuwapo kwa mipango ya kuendeleza vipaji vya vijana.
Kiemba akiwajibika uwanjani kwenye mechi za Ligi Kuu
Kiemba akionyesha manjonjo yake
CHIMBUKO
Kiemba anaitaja Klabu ya Kagera Sugar kama ya mafanikio kwake, huku akiwataja walimu Malume na Kabuta waliomnoa kwenye michezo ya Umishumta na Idd Kipingu aliyempokea Shule ya Sekondari Makongo, kuwa ni watu asiowasahau kwa kukuza kipaji chake.
"Siwezi kuwasahau watu hawa kwa walivyosaidia kukuza na kuendelea soka langu," anasema.
Nyota huyo aliyewaasa wachezaji wenzake kuzingatia miiko na maadili ya uchezaji ili wacheze kwa muda mrefu, alizaliwa mwaka 1983 mjini Kigoma akiwa ni mtoto wa pili kati ya watano wa familia yao iliyokuwa na watoto wa kiume watatu na wa kike wawili.
Alisoma Shule ya Msingi Burka, Arusha alipoanza kuonyesha kipaji chake cha soka akiteuliwa katika timu ya shule na timu za Mkoa wa Arusha kwenye michuano ya Umishumta akishiriki fainali tatu za taifa kuanzia 1997-1999.
Chandimu alicheza katika timu ya Small Tiger na timu yake ya kwanza ya ligi ni Home Boys ya Arusha kabla ya kujiunga Shule ya Makongo alipoteuliwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana ya U-17, wakati akiwa anaichezea pia Karume Rangers.
Aliondoka Karume iliyokuwa na maskani yake Mbeya ikifahamika pia kama 44 KJ na kwenda kwa muda Pallsons ya Arusha, kisha kukimbilia Kagera Sugar aliyosaidia kuipandisha Ligi Kuu mwaka 2005 na kuonwa na Yanga iliyomnyakua msimu wa 2006/2007.
Aliachana na Yanga na kwenda Zanzibar kuichezea Miembeni kwa muda na kurejea Bara kujiunga na Moro United hadi msimu wa 2009/2010 aliponyakuliwa na Simba aliko hadi sasa.
Mafanikio yake kama mchezaji, Kiemba anasema ni kutwaa mataji kadhaa yakiwamo ya Ligi Kuu, Mapinduzi na Tusker akiwa na timu za Simba na Yanga.

No comments:

Post a Comment