STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, January 23, 2014

CCM yaonya watendaji wa serikali 'mizigo'


Mara baada ya kuundwa kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inayoongozwa na Katibu Mkuu Ndg. Abdulrahman Kinana mwanzoni mwaka mwaka jana, Sekretarieti hiyo imejiwekea utaratibu wa kufanya ziara mikoani kukutana na wananchi kusikiliza kero zao,kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuimarisha Chama mikoani. Utaratibu huu ni agizo la mkutano mkuu wa Taifa wa nane wa CCM uliofanyika Novemba 2012 mjini Dodoma. Nanukuu azimio hilo;
 
“ Chama Cha Mapinduzi lazima kiwe karibu na wananchi, kisikilize changamoto zao na kiwasemee wananchi na hasa wanyonge” Moja ya maazimio ya Mkutano Mkuu wa nane wa CCM 2012.
 
Kwa hiyo msingi wa kwanza wa ziara hizo ni maagizo ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ambacho ndicho kikao cha juu kabisa cha Chama. Msingi wa pili ni ukweli kuwa CCM ndio iliyopewa dhamana na kuingia mkataba na wananchi kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015, hivyo inayowajibu wa kukagua utekelezaji wa ilani hiyo.
 
Na bila shaka wote tumeshuhudia jinsi ziara hizo zilivyoinua uhai wa Chama nchi nzima na kuongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kutatua kero mbalimbali za wananchi kwenye maeneo yao, kiasi cha kuongeza imani ya wananchi kwa CCM.
 
Tumeshuhudia makundi mbalimbali ndani ya jamii yakija kueleza changamoto zao ndani ya Chama. Makundi hayo ni pamoja na makundi ya wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, wanafunzi na wafanyakazi hasa walimu. Huu ni uthibitisho wa kuongezeka kwa imani yao kwa CCM.
 
Katika mwendelezo wa ziara hizo mwishoni mwa mwaka jana Katibu Mkuu wa CCM na baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti walifanya ziara ya siku 26 katika mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe. Pamoja na mambo mengine wananchi walilalamikia baadhi ya watendaji wa serikali hasa baadhi ya mawaziri wakiamini kuwa yapo mapungufu kadhaa yanayotokea kwenye wizara zao.
 
CCM kama lilivyo agizo la Mkutano mkuu la kuwasemea wananchi tulisikiliza kilio chao na kwa kufuata utaratibu, baadhi ya mawaziri hao waliitwa na kuhojiwa kwenye Kamati Kuu ya CCM mwezi Disemba 2013.

 Utaratibu wa watendaji wa serikali kutoa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye vikao vya Chama sio mgeni na wala haujaanza jana. Wakuu wa wilaya hutoa kwenye wilaya, wakuu wa mikoa hutoa mikoani kwao,hivyo sio utaratibu mpya.
 
Baada ya mahojiano hayo Kamati Kuu ya CCM ilitoa ushauri kwa serikali wa namna ya kurekebisha mapungufu yaliyoelezwa na wananchi. Kwakuwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi mwenye mamlaka na mawaziri ni Rais mwenyewe, CCM ililiacha suala hili kwake aangalie njia ipi bora ya kuondoa mapungufu tuliyoyaeleza.
 
Na kwenye taarifa yetu kwa vyombo vya habari baada ya kikao hicho tulisisitiza kuwa sio lazima awafukuze mawaziri husika isipokuwa wanaweza kufanya mabadiliko katika mfumo,sheria nk ili mradi kuwepo na mabadiliko katika kushughulikia mambo yaliyolalamikiwa na wananchi.
 
Hivi karibuni Rais amefanya mabadiliko kidogo kwenye baraza lake la mawaziri na kuwarudisha baadhi ya mawaziri waliolalamikiwa na wananchi na wabunge, ambao malalamiko hayo yaliungwa mkono na CCM. Ni kupitia malalamiko hayo ndipo lilipozaliwa jina la mawaziri mizigo. Baada ya uteuzi huo kukaibuka mjadala mkubwa nchini wakihoji kulikoni Rais kaamua kutowatimua mawaziri hao.
 
Kwanza haikua hoja ya CCM kuwafukuza mawaziri hao bali kuchukua hatua za kurekebisha mapungufu husika. Kufukuza inaweza kuwa ni njia ya kutatua tatizo lakini sio njia pekee. Hivyo basi CCM tunaamini kuwa kurudishwa kwao wamepewa fursa ya kurekebisha mapungufu tuliyoyasema kwa niaba ya wananchi. Tunaamini mawaziri wote hawatabweteka bali watatimiza wajibu wao na kuhakikisha wanawatumikia wananchi ambao ndio waajiri wa serikali.
 
Ifahamike kuwa Chama Cha Mapinduzi hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha mapungufu na watakaoshindwa kutimiza wajibu wao vizuri. Wakumbuke kushindwa kwao kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa Ilani ya uchaguzi ya CCM, CCM haitavumilia usaliti huo. Kukaa kimya kwa CCM itakua ni kujinyonga yenyewe jambo ambalo hatutaruhusu kabisa.
 
Tunajua wapo baadhi ya watendaji wa serikali wasiopenda kuhojiwa utendaji wao, tunawasihi kwa moyo safi wasiotaka kuulizwa juu ya utendaji wao waondoke serikalini wenyewe kwani CCM tutakuwa wakali sana kwenye mapungufu,kwani tukikaa kimya tutakua tunajihujumu wenyewe.
 
Tutatumia vizuri wingi wa wabunge wetu bungeni na wingi wa madiwani wetu kwenye halmashauri kuisimamia vizuri serikali. Hivyo kuanzia sasa kasi ya CCM kuisimamia serikali, kuisifu itakapofanya vizuri na kukosoa itakapofanya vibaya itaongezeka mara dufu kwa kila ngazi.
 
Tunawaomba watanzania kwa ujumla tuwape muda wateule hawa wa Rais watimize wajibu wao, lakini tusisite kusema pale tutakapoona mambo hayaendi kama tunavyotarajia. Uwajibikaji wa kweli ndio msingi wa mafanikio na maendeleo yetu.
 
CCM inawatakia kila lakheri kwenye kutimiza wajibu wao. Tuna matumaini makubwa kuwa wote kwa pamoja hawataisaliti ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba hawatayaangusha matumaini ya wananchi kwa serikali yao.
 
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
 
Imetolewa na;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
23/01/2014

No comments:

Post a Comment