STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, December 6, 2010

Mkulo: Nimewasamehe walionichafua, ila sintowasahau

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Mustafa Mkulo, amesema pamoja na kuwasamehe wale wote waliompakazia mabaya wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, bado hawezi kuwasahau hadi anaingia kaburini.
Pia, amewataka wanachama wa CCM na wananchi wa Kilosa kwa ujumla, kuzika tofauti zao zilizosababishwa mchakato wa uchaguzi mkuu, ili kuweza kushikamana kuijenga wilaya na jimbo lao la Kilosa liweze kuwa mfano wa kuigwa nchini.
Akizungumza kwenye mapokezi na hafla ya kupongezwa kuteuliwa tena kuwa waziri, Waziri Mkulo, alisema kashfa alizokuwa akipewa akidaiwa sio raia wa Tanzania na kejeli zingine ni vitu ambavyo vilimuumiza, ila amewasamehe wote waliomfanyia jambo hilo.
Waziri alisema hata hivyo pamoja na kuwasamehe wahusika, katu hatawasahau kwa vile walimpa wakati mgumu na kumnyima raha, kitu alichodai kitaendelea kubaki kichwani mwake hadi kifo.
Alisema wale walioanzisha na kueneza maneno hayo na waliomtusi, wasimuogope kwa sababu anafahamu siasa ni mchezo usio na simile na wenye kuhitaji uvumilivu mkubwa kitu alichoweza kukimudu na ndio maana amewasamehe kwa yote.
"Walionitusi na kunizushia kwamba mie sio raia na wengine kufikia hata kumhusisha mke wangu, wote nimewasamehe, ila kwa hakika sintowasahau, muhimu nataka kuwaambia wahusika wasiwe na hofu juu yangu yale yamepita kwani najua siasa ndivyo zilivyo," alisema Mkulo.
Alisema kama sio mambo ya siasa, kwa hakika angeweza kuwafungulia mashtaka na kudai fidia kubwa wahusika wote waliomchafua kipindi cha kura za maoni ndani ya CCM na hata kwenye uchaguzi mkuu uliompa ushindi wa kishindo yeye Mkulo na chama chake.
Waziri Mkulo, alisema kwa kuwa uchaguzi umeshapita kwa sasa yeye ni mbunge wa wakazi wote wa Jimbo la Kilosa na hivyo atawatumikia wananchi wote kwa ajili ya kuwaletea maendeleo, akiomba kupewa ushirikiano wa kutosha kufanikisha aliyopanga kwa miaka mitano ijayo.
Wakati wa mchakato wa kura za maoni, Waziri Mkulo alivumishiwa kuwa yeye si raia wa Tanzania na kikundi cha watu waliojiita Wazee wa Kilosa, ambao walikuja kurukwa na uongozi wa Baraza la Wazee la wilaya hiyo waliodai hawakumtuma mhusika aliyeanzisha chokochoko hizo.
Pia baada ya kushinda kiti hicho cha Ubunge kwa mara ya pili, baadhi ya watu walidaiwa kuapa kuwa asingekuwa miongoni mwa wateule wa Baraza Jipya la Mawaziri, kitu kilichoenda kinyume kutokana na Rais Jakaya Kikwete kumtangaza kuendelea kushikilia wizara hiyo ya Fedha.

No comments:

Post a Comment