STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 4, 2011

TAFF yapewa kifyagio kwa tamasha la filamu la Nyerere

SHIRIKISHO la Filamu Tanzania, TAFF, limepewa heko kwa ubunifu wake wa kuanzisha tamasha la filamu za Kibongo ambalo litafanyika Februari 14-19 jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo la kwanza kufanyika nchini kwa filamu za Kitanzania litafanyikia kwenye viwanja vya Leaders kwa kuzunduliwa na Rais Jakaya Kikwete na kufungwa na mke wa hayati baba wa taifa, Mwl Nyerere, Mama Maria Nyerere.
Baadhi ya wadau wa filamu wakiwemo wasanii wa fani hiyo wamesema kitendo cha TAFF kubuni tamasha hilo ni jambo la kupongezwa kwa vile litasaidia kuinua soko la kazi za wasanii wa kibongo, mbali na kutoa fursa kwa wananchi kupata mwamko wa kuzipenda kazi hizo.
"TAFF wamefanya jambo la maana ambalo wadau wa filamu Bongo tulikuwa tunalisubiri kwa muda mrefu, kitu cha muhimu waliendeleze kama mengine," alisema Leila Mwambungu wa Kimara.
Leila, alisema tamasha hilo linaweza kusaidia kuamsha hisia wa watanzania kupenda kazi za nyumbani kwa madai wapo wengine wanazichukulia poa filamu za Kibongo na kuhusudu kazi za Nigeria au Marekani.
Mtayarishaji wa filamu anayekuja juu, Husseni Ramadhani 'Swagger' alisema tamasha hilo ni kama njia ya wadau wa filamu kujitangaza na kuwahimiza wenzake kujitokeza kwa wingi kulishiriki kuanzia mwanzo wake hadi siku ya ufungwaji wake.
"Nafasi kama hizi ni muhimu kuzichangamkia, kwa kweli nalipongeza TAFF kwa kubuni kitu kama hiki, kwani itatusaidia wengine kujifunza makubwa zaidi ya yale tunayoyajua katika sanaa hiyo kutokana na ukweli tumesikia kuna mafunzo kadhaa yatakayotolewa hapo," alisema Swagger ambaye anatamba na filamu kama Hazina, Who is a Killer na sasa Bangkok Deal.
TAFF kupitia viongozi wake chini ya Rais Simon Mwakifamba, walitangaza kuanzisha kwa tamasha hilo litakalozinduliwa wiki ijayo na Rais Kikwete kwa ajili ya kuonyesha kazi za kitanzania pamoja na kupambwa na burudani kadhaa za sanaa na mada mbalimbali za kifani.
***

No comments:

Post a Comment