STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 30, 2012

Azam yakana kuchunguza kipigo cha Yanga

WAKATI taarifa zilizagaa jana kwamba Azam imewasimamisha wachezaji wake wawili Mrisho Ngassa na Salum Aboubakar 'Sure Boy' kwa tuhuma za kucheza chini ya kiwango dhidi ya Yanga katika fainali ya Kombe la Kagame waliyolala 2-0 Jumamosi na kwamba nyota wengine watatu Aggrey Morris, Said Morad na kipa Deogratius Munishi 'Dida' wanachunguzwa, uongozi wa klabu hiyo ya Chamazi umesema walifungwa kihalali na hakuna mchezaji wa wanayemtuhumu kwa chochote. Afisa Habari wa Azam FC, Jaffer Idd alisema Yanga walitumia makosa machache yaliyofanywa na mabeki wa Azam na kupachika mabao yaliyowapa ushindi wana Jangwani hao. "Timu yetu ilicheza vizuri kwenye mechi ya fainali lakini Yanga ilituzidi ujanja na kutumia vizuri nafasi chache walizopata," alisema Jaffer. Alisema hawawezi kumlaumu mchezaji yeyote kwa kipigo hicho kwa sababu wachezaji walioifikisha fainali timu hiyo ndio waliocheza mechi hiyo ya fainali na akawasifu wachezaji wa timu hiyo kwa ushujaa wa kuifikisha Azam fainali licha ya kwamba ilikuwa ikishiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza. Jaffer alisema uongozi wa Azam umeridhika na matokeo hayo na kwamba sasa wanaelekeza nguvu zao katika maandalizi ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika. Akizungumza na gazeti hili jana, Ngassa alisema kuwa timu yake juzi haikuwa na bahati ya kutwaa ubingwa huo lakini wanamshukuru Mungu kwa kufika fainali. Ngassa alisema kwa dakika chache alizopewa kucheza, zikiwemo za mechi ya fainali alijituma na kuisaidia timu yake. "Sidhani kama kuna aliyecheza chini ya kiwango, tumejituma na tumefika mbali licha ya kutochukua ubingwa," alisema Ngassa na kuongeza kwamba hajasimamishwa na uongozi wa timu yake kama ambavyo ilikuwa inazungumzwa jana. Ilidaiwa pia kwamba uongozi wa Azam haukufurahishwa na kitendo cha Ngassa kwenda upande wa mashabiki wa Yanga na kushangilia baada ya kufunga goli kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wachezaji wa Azam wamepewa mapumziko ya siku mbili ambapo kesho wataanza mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

No comments:

Post a Comment