STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, July 30, 2012

Batungi: Mkali wa Kikapu achekeleaye ajira jeshini

LICHA ya mchezo wa kikapu kumpatia rafiki wengi na kufahamika ndani na nje ya nchi, nyota wa klabu ya ABC, Gilbert Batungi 'B10' amesema kitu kikubwa anachojivunia kupitia mchezo huo ni elimu na ajira aliyopata jeshini. Batungi, aliyeingia kwenye kikapu kwa ushawishi wa kaka yake aitwaye Jerome, alisema ajira hiyo aliipata mwaka 2006 kutokana na umahiri wake dimbani. Alisema anaifurahia ajira hiyo kwa vile hakuwahi kuiota kuja kuipata maishani mwake. Batungi, anayemudu nafasi ya kati, alisema pia kikapu kilimwezesha kupata nafasi ya kusoma Shule ya Sekondari Jitegemee baada ya kung'ara katika UMISSETA mwaka 2000 iliyofanyikwa jijini Mwanza. Alisema wakati akishiriki michuano hiyo alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Binza, kwa jinsi alivyong'ara aliuvutia uongozi wa Jitegemee iliyomchukua akiwa kidato cha pili na kusoma hadi alipohitimu kidato cha nne. Alisema kutua kwake Jitegemee kulimwezesha kuonwa na kuitwa timu ya mkoa wa Dar tangu mwaka 2001 na ile ya taifa 2005 na kuzichezea mpaka sasa bila kutarajia. Juu ya pambano gumu alilowahi kukutana nalo, Batungi apendae kula ugali kwa dagaa na mboga za majani na kunywa juisi ya embe, alitaja mchezo wa mwaka 2005 kati ya Tanzania na Kenya wa kuwania ubingwa wa Afrika Mashariki. "Naikumbuka mechi hii kwa vile ilikuwa mara yangu ya kwanza kuichezea timu ya taifa, pia licha ya ugumu wake niliisaidia Tanzania kuilaza Kenya kwa mara ya kwanza." Alisema mchezo huo uliochezwa Nairobi na kuisha kwa Tanzania kuiduwaza Kenya kwa vikapu 61-60. "Hakika mafanikio niliyopata katika mechi hiyo hasa kuaminiwa na makocha na kutiwa moyo na wachezaji wenzangu, ni jambo linalonifanya nisiisahau," alisema. Batungi, aliyekuwa mmoja wa wawaniaji wa Tuzo za TASWA za 2012 kama Mchezaji Bora wa Kikapu kwa mara ya pili mfululizo, alisema safari yake ya michezo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na makundi matatu ya watu asiowasahau milele. Alitaja kundi la kwanza ni wazazi wake waliomuunga mkono kwa kumtia moyo tangu utotoni, pili makocha wote waliomfundisha katika timu tofauti, na wachezaji wenzake waliomtia nguvu kwa kukitambua kipaji chake katika mchezo huo. "Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sintowashukuru watu hawa kwa hapa nilipofika," alisema. Batungi, aliyetwaa ubingwa wa Majiji akiwa na timu ya mkoa wa Dar 'The Dream Team', ubingwa wa Taifa wa Kikapu (NBL) na ule wa Muungano akiwa na klabu ABC ni mnazi mkubwa wa soka mchezo alioupenda kabla ya kaka yake kumbadilisha. Ni shabiki mkubwa wa klabu za Chelsea na Simba akivutiwa na kiungo Mwinyi Kazimoto na Didier Drogba. B10 Mkali huyo alitoboa siri ya jina lake la utani la 'B10', akisema ni kifupi cha ubini wake na jezi namba 10 anayopenda kuivaa tangu alipoibukia katika kikapu mwaka 1998. "Naipenda mno jezi namba 10, nimekuwa nikiivaa tangu naanza kucheza kikapu na ndio maana wengi huniita B10, ikimaanisha Batungi Namba 10," alisema Batungi, anayechizishwa na rangi nyekundu na nyeupe akimzimia nyota wa kikapu nchini Abdallah Ramadhani 'Dullah', alisema ndoto zake ni kuiona Tanzania ikitamba kimataifa na kuwasaidia vijana chipukizi kuja kuvaa 'viatu' vyao mara wakistaafu. Nyota huyo anayependa kucheza Pooltable, alisema mchezo wa kikapu umedidimia kwa kukosekana viongozi makini na wenye uchungu na mchezo huo. Alisema wengi wa viongozi wa sasa ni wababaishaji wanaojali masilahi yao na ndio waliochangia hata wadhamini kuukimbia mchezo huo na kutoa rai kwa wadau wenzake kubadilika kwa kuwachagua watu makini. "Tusipozinduka na kuchagua watu wenye mapenzi na uchungu na kikapu, tutarajie mchezo huo kudidimia zaidi," alisema. Alidai kama angekutana na Rais au Waziri wa Michezo, angeomba serikali isaidie michezo yote badala ya kuangalia soka tu, pia angeiomba ishinikize makampuni kuwekeza kwenye michezo kwa kusaidia udhamini. "Pia ningeiomba serikali iwekeze nguvu katika michezo ya vijana ili kusaidia taifa kuwa na nyota wa baadae kwa michezo yote ili itambe kimataifa," alisema. Batungi, ambaye hajaoa ila ana mtoto mmoja, alisema hakuna ujinga anaoujutia kama tabia aliyokuwa nayo enzi akiibuka katika kikapu ya kutega mazoezi magumu kwa kusingizia ugonjwa alipokuwa akisoma Jitegemee. Alisema kitu kinachomhuzunisha ni kifo cha nyota wa Netiboli, Grace Daudi 'Sister' na kudai kitu kimngine anachokifanya nje ya ajira yake jeshini ni biashara ya kuuza nguo. ALIPOTOKA Gilbert Paul Batungi, alizaliwa Januari 5, 1983 mkoani Shinyanga akiwa wa sita kati ya watoto saba wa familia yao. Alisoma Shule ya Msingi Binza ya Maswa-Shinyanga na kuendelea na masomo ya Serkondari Shule ya Binza na baadae Jitegemee. Kimichezo alianza kucheza soka na kutamba katika timu ya shule kabla ya kaka yake kumshawishi kucheza kikapu ambapo aliianza kuucheza rasmi mwaka 1998 katika klabu ya Black Wizard ya Shinyanga. Baada ya kung'ara katika UMISSETA mwaka 2000 iliyofanyika Mwanza na kuonwa na Jitegemee alihamia jijini Dar na kupata fursa ya kuzichezea timu za Mgulani JKT, Chang'ombe Boys na Vijana. Mwaka 2004 akiwa ameshamaliza masomo yake ya Sekondari, aliitwa JKT Mgulani kama mchezaji wa kiraia na miaka miwili baadae akapata fursa ya kuwa miongoni mwa walioajiriwa jeshini na kuhamia timu ya ABC anayoichezea mpaka sasa. Batungi, anayetamani kuwa na watoto wawili pale atakapooa, aliwakumbusha wachezaji wenzake kujibidiisha kufanya mazoezi na kuwa makini na ugonjwa wa Ukimwi aliodaai unapoteza nguvu kazi kubwa ya taaifa. Alisema rai hiyo ya kujikinga Ukimwi sio kwa wachezaji tu bali jamii kwa ujumla kwa kuitaka kuepuka ngono zembe, wawe waaminifu na kutumia kinga, huku akisisitiza kinga sahihi ni kufanya ibada na kufanya mazoezi ili kupunguza mihemko. Aliwasihi wachezaji wenzake kujituma uwanjani na kuwa na nidhamu ili kusaidia kushawishi wadhamini kuwasaidia.
Mwisho

No comments:

Post a Comment