STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 5, 2012

Eddo Boy: Kinda la Simba achekeleaye kuitungua Mtibwa Sugar

LICHA ya kuibuka mfungaji bora wa michuano ya Super8, mshambuliaji kinda wa Simba, Edward Christopher Shija 'Eddo Boy' a.k.a Teko Modise, amedai hajafurahishwa kama alivyoibebesha timu yake ubingwa wa michuano hiyo. Eddo, alisema tuzo ya ufungaji bora kwake isingekuwa na maana kama Simba isingekuwa mabingwa kwa jinsi walivyojituma na kuipigania timu yao. "Ingawa mechi ya fainali dhidi ya Mtibwa Sugar kwangu ni mechi ngumu kuwahi kuicheza kwa jinsi ilivyokuwa na funga nikufunge, ila sijivunii tuzo ya ufungaji bora wala kung'ara kwangu zaidi ya kuipa Simba ubingwa," alisema. Alisema, mara pambano lilipoisha akiifungia bao la ushindi katika matokeo ya mabao 4-3, alijisikia faraja kwa kutwaa taji jingine akiwa na Simba. "Mechi na Mtibwa sintoisahau kwa walivyocheza na kurejesha mabao yetu kila tulipofunga kabla ya kuwazidi ujanja kwa bao la nne lililotupa ubingwa, hakika najisikia fahari kwa kuilaza Mtibwa na kuipa Simba taji jingine," alisema. Kabla ya taji hilo, Eddo alishatwaa na Simba mataji ya Rolling Stone 2011, Kinesi 2011, Uhai 2011 na Ujirani Mwema lililochezwa mwaka huu. Pamoja na mafanikio yote, Eddo anayeichezea pia timu ya taifa, akipandishwa mwaka huu na kocha Kim Poulsen toka timu ya U20, alisema habweteki wala kulewa sifa. "Siwezi kulewa sifa kwa mafanikio niliyonayo kwa kipindi kifupi, ndoto zangu nije kucheza soka la kulipwa Ulaya na kutamba kimataifa," alisema. LUNYAMILA Eddo, alizaliwa Septemba 10, 1992 mjini Tabora akiwa mtoto wa pili kati ya watatu kwa familia iliyolelewa na mama pekee. Elimu ya Msingi aliisoma Shule za Choma Chankola,Tabora na Mwele ya Morogoro, kabla ya kujiunga na Sekondari za St Francis na baadae Makongo. Kisoka alianza kutamba tangu akiwa darasa la tatu akiwa Morogoro, timu yake ya chandimu ikiwa ni Jamhuri Ball Boys na baadae Moro Kids iliyowakusanya baadhi ya nyota wanaotamba kwa sasa nchini. Alisema wakati akichipukia alivutiwa na baadhi ya nyota wa zamani wa Simba na Yanga kama Edibily Lunyamila, Salvatory Edward, Mark Sirengo na Nteze John wa Simba, huku akimtaja kocha Yahya Belini kama mtu aliyekigundua na kukiendeleza kipaji chake. Eddo alisema safari yake kisoka ilipata vikwazo vingi toka kwa mama yake aliyekuwa hapendi kabisa acheze, kiasi cha kumchapa, kumnyima chakula na hata kumfungia na kulala nje pale alipomkaidi na kujihusisha na soka. "Mama yangu aliyekwishafariki hakupenda nicheze soka, ila nilikuwa nunda na kuishia kulambwa bakora, kunyimwa chakula na hata kufungiwa mlango na kulala nje, ingawa sikukata tamaa," alisema. Alisema jambo zuri ni kwamba kabla mama yake hajafariki mwaka 2005 alishaanza kusikia sifa zake kisoka toka kwa shoga zake na kumuacha acheze hasa alipohamia Makongo jijini Dar es Salaam. Eddo, aliyedai hajaonana na baba yake mzazi tangu mwaka 1998 baada ya kutengana na marehemu mama yao, alisema roho inamuuma kuona mamaye akifa bila kula jasho lake kisoka. YANGA B Eddo, anayependa kula vyakula vyote na kunywa vinywaji laini, alisema safari yake kisoka alipohamia Dar aliwahi kuichezea Yanga B aliyokuja kuachana nayo baada ya kuona hawana muelekeo wowote wa kimaendeleo.maendeleo. Alisema alienda Yanga baada ya kuisaidia Kinondoni kutwaa ubingwa wa Copa Coca Cola mwaka 2007 na kisha kuifikisha timu ya Kinondoni katika fainali za Taifa na kulazwa na Ilala mabao 5-0. Alisema alipoachana na Yanga alirejea darasani katika Shule ya Lord Baden Powell kabla ya kutimkia Moro United B aliyoichezea kabla ya kutua Miundo Mbinu ya Lindi aliyoipandisha daraja la kwanza na kuichezea timu ya mkoa wa Lindi katika michuano ya Kombe la Taifa 2009. Alisema mara baada ya fainali hizo na Lindi kufungwa na Singida, ndipo aliponyakuliwa na Simba kung'ara nao akinyakua mataji na tuzo mbalimbali hadi kupandishwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo msimu uliopita. Eddo anayezishabikia Arsenal, Barcelona, Orlando Pirates na Brazil akiwazimia Neymar, Samuel Etoo na Ronaldo de Lima, alisema soka limempa mafanikio mengi kisoka na maisha ingawa hakupenda mambo yake yaanikwe. "Soka limenisaidia mengi, ila sipendi kila mtu ajue, najivunia na kiu yangu ni kung'ara zaidi nicheze soka la kulipwa Ulaya, safari yangu bado kabisa Simba sio mwisho wangu," alisema. Eddo ambaye hajaoa wala kuwa na mtoto, ingawa angependa kuwa na watoto watatu atakapooa, alitoa wito kwa wachezaji wenzake kujituma, kujiamini na kuwa na nidhamu waweze kufika mbali. Pia aliwakumbusha viongozi wa soka nchini kubadilika na kuachana na tabia ya kutumia nguvu na fedha nyingi kuwapapatikia 'mapro' wa kigeni na badala yake kuwekeza katika soka la vijana ili kulisaidia taifa hapo baadae. "Mafanikio ya kikosi cha Simba B ni funzo kwa viongozi na wadau wa soka nchini wawekeze katika soka la vijana badala ya kupigana kumbo kugombea mapro wa nje, fedha wazitumiapo kwao zisaidie soka la vijana," alisema. Eddo anayetamani kuwa mfanyabiashara mkubwa atakapostaafu soka na anayependa muziki wa reggae akimzimia J Booge, Biggy Signal na P Square, aliwashukuru mama yake, makocha wote waliomnoa na rafiki na wachezaji wenzake kwa kufika hapo alipo. Nyota huyo asiyeamini mambo ya uchawi katika soka akiamini mazoezi ndio kila kitu, alisema angekutana na Rais au waziri wa michezo angewaomba zijengwe na kuanzishwa shule maalum za michezo. pia kutaka soka la vijana lipewe kipaumbele zaidi. Mwisho

No comments:

Post a Comment