STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 5, 2012

Kimobiteli arejea Extra Bongo, atua na moja mpya

BENDI ya muziki wa dansi ya Extra Bongo imemrejesha kundini aliyekuwa muimbaji wao Khadija Mnoga 'Kimobitel' aliyekuwa ametimkia African Stars 'Twanga Pepeta'. Uongozi wa Extra Bongo ulisema umemrejesha kundini mwanamuziki huyo baada ya mwenyewe kuridhia kurudi huku bendi yao ikiwa ina upungufu mkubwa katika safu ya uimbaji kwa sauti ya kike. Mkurugenzi wa Extra, Ally Choki, alisema wakati wa kumtambulisha muimbaji huyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa kurejea kwa Kimobitel kutasaidia kuimarisha safu yao ya uimbaji. Choki alisema Kimobitel aliyeikacha Extra Bongo miezi kadhaa iliyopita amerejea kundini akiwa na 'zawadi' kwa mashabiki kwa kuja na wimbo mpya uitwao 'Mgeni'. Mkurugenzi huyo alisema Extra Bongo inatarajiwa kumtambulisha rasmi Kimobiteli kwa mashabiki wiki ijayo baada ya kufanya mazoezi ya kutosha na wenzake. Kimobitel alisema amerejea Extra Bongo bila kulazimishwa na mtu huku akidai bendi aliyotoka hakuwa na mkataba wowote na hivyo anawaomba mashabiki wa bendi hiyo wampokee na watarajie mambo mazuri kutoka kwao. "Nimeamua mwenyewe kurejea Extra Bongo, na yale yaliyopita yamepita tuangalie mapya ninachoomba mashabiki wetu wasubiri vitu adimu toka kwangu," alisema. Mwanadada huyo aliyewahi kutamba na bendi mbalimbali ikiwemo African Revolution na Double M Sound, alisema anaamini aliwakwaza watu alipoondoka Extra Bongo, lakini ni suala la kusameheana kwani ametambua alipotoka na amerejea nyumbani akihitaji kupokelewa vema. Naye kiongozi wa bendi hiyo, Rogart Hegga 'Katapila' alisema wana Extra Bongo wamefurahishwa na ujio wa Kimobitel akidai bendi yao sasa imekamilika vya kutosha hasa baada ya kushindwa kuziba pengo la mwanamuziki huyo tangu alipoondoka. Alisema licha ya kwamba mwanamuziki huyo atatambulishwa rasmi wiki ijayo, lakini bendi yao itaendelea na maonyesho yao kama kawaida wiki hii kwa siku za Ijumaa na Jumapili kufanya vitu vyao White House-Kimara na Jumamosi Meeda Club, Sinza. Mara baada ya utambulisho wa mwanamuziki huyo kwa waandishi, alitambulishwa pia kwa wanamuziki wote wa Extra Bongo ambapo kwa kauli moja wanamuziki hao walimpokea na kumkaribisha nyumbani wakimuahidi ushirikiano ili bendi yao izidi kupaa.

No comments:

Post a Comment