STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, September 28, 2012

KOCHA MPYA YANGA AWASILI KIMYAKIMYA

Brandts

Na Mahmoud Zubeiry
KOCHA mpya wa Yanga, Ernstus ‘Ernie’ Wilhelmus Johannes Brandts, beki wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya PSV Eindhoven ya Holanzi, atawasili wakati wowote kuanzia leo kusaini mkataba na kuanza kazi katika klabu hiyo.
Hata hivyo, Yanga imeamua kufanya siri ujio wa kocha huyo, kwa sababu haitaki mapokezi ya mbwembwe, kutokana na rekodi yake ya kutodumu na makocha.
Yanga, imetimiza malengo yake ya kuwa kocha mpya, kabla ya kucheza na wapinzani wao wa jadi, Simba SC, Oktoba 3, mwaka huu baada ya kumfukuza Mbelgiji, Tom Saintfiet, kutokana na kufikia makubaliano na Brandts.
Mholanzi huyo aliyefukuzwa APR ya Rwanda baada ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Agosti mwaka huu amepewa ukocha wa Yanga, baada ya Mbrazil Marcio Maximo kukataa nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Mtaalamu huyo, alizaliwa Februari 3, mwaka 1956 mjini Nieuw-Dijk, Gelderland, mbali na PSV Eindhoven, alichezea pia Roda JC Kerkrade, MVV Maastricht na De Graafschap.
Brandts aliichezea mechi 28 timu ya taifa ya Uholanzi na kuifungia mabao matano na pia alicheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978.
Katika fainali hizo, Raundi ya pili kwenye mechi na Italia, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyezifungia mabao timu zote katika mechi moja kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Alianza kujifunga dakika ya 18, kisha akaisawazishia Uholanzi dakika ya 50 katika mechi ambayo, mchezaji mwenzake Arie Haan baadaye aliifungia timu yake bao la ushindi na kutoka kifua mbele kwa mabao 2–1.
Alipostaafu soka akawa kocha na katikati ya msimu wa 2007–2008, Brandts aliambiwa hataongezewa mkataba NAC-Breda, licha ya matokeo mazuri ya kushika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Uholanzi (Eredivisie), ingawa uamuzi huo haukuwafurahisha mashabiki wa timu hiyo na nafasi yake akapewa Robert Maaskant kuanzia msimu wa 2008–2009.
Akateuliwa kuwa Kocha wa Rah Ahan mwaka 2009, kabla ya kufukuzwa Desemba 2009 na kuibukia APR ya Rwanda mwaka 2010, ambako ‘riziki’ yake imeisha miezi miwili iliyopita na sasa amepata maisha mapya Yanga.
Akiwa APR, Brandts alifungwa mechi zote mbili na Yanga iliyokuwa ikifundishwa na Mbelgiji Tom Saintfiet katika Kombe la Kagame, moja ya makundi 2-0 na nyingine ya Nusu Fainali 1-0. Yanga iliibuka bingwa, ikiifunga Azam FC 2-0 kwenye fainali.
Brandts atakutana na wachezaji wake wa zamani wawili Yanga, beki Mbuyu Twite anayeanza msimu wa kwanza katika klabu hiyo na kiungo Haruna Niyonzima anayeingia katika msimu wa pili, ambao alifanya nao kazi APR.
 
CHANZO:BIN ZUBEIRY

2 comments:

  1. Ingekuwa mapenzi yangu Yanga isingeleta tena kocha wa kigeni kwa sababu watajitia aibu na kuitia doa soka la Tanzania na mtindo wao wa kuwatimua kila mara.

    ReplyDelete
  2. YANGA WAMUANNGALIE MWENYEKITI WAO NAHISI KAMA ANAPIGIA MAHESABU JENGO LA MAFIA NDIO MAANA ANAWALETA MAKOCHA WA KIGENI NA KUINGIA NAO MIKATABA KISHA ANAWATIMUA KWA KUKIUKA MIKATABA KISHA ANATOA FEDHA ZAKE MWENYEWE MWISHOE KUJA KUIDAI YANGA, ITAFIKIA DENI LAKE KWA YANGA LIWE KUBWA NA KUTOA OPTION YA KUUZIWA JENGO LA MTAA WA MAFIA ILI AENDESHE SHUGHULI ZAK...HUYU JAMAA HATABIRIKI NA NI KAMA MWENYE ALEJI NA MAJENGO

    ReplyDelete