STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, October 13, 2012

Kiemba akana kuziba pengo la Mafisango Simba

Amri Kiamba akishangilia bao moja ya mabao yake katika Ligi Kuu msimu huu

KIUNGO nyota wa Simba, Amri Kiemba, licha ya kuwashukuru mashabiki wa klabu hiyo kumfananisha na kiungo wa kimataifa wa timu hiyo Patrick Mafisango, aliyefariki kwa ajali ya gari Mei mwaka huu, amekiri hajaliziba pengo la kiungo huyo.
Akizungumza na MICHARAZOE muda mchache kabla ya kuondoka jijini na kikosi cha timu yake kuelekea Tanga kuwahi pambano lao dhidi ya Coastal Union, Kiemba alisema licha ya kuanza msimu kwa kung'ara, bado anajiona hajaliziba pengo la Mafisango hata kama watu wanaridhika na kiwango chake.
Kiemba, alisema ni vigumu pengo la kiungo huyo aliyefariki Mei 17 kuzibika kirahisi na kwa ukamilifu kutokana na uwezo na kipaji kikubwa alichokuwa nacho nyota huyo kutoka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
"Nashukuru mashabiki kuridhika na juhudi zangu uwanjani kiasi cha kuona kama nimeziba pengo la Mafisango, ila ukweli ni vigumu pengo la kiungo huyo kuzibika kirahisi hata mie mwenyewe najiona sijaliziba hata kidogo, " alisema
Kiemba aliongeza, binafsi alikuwa akimkubali Mafisango kwa umahiri wake hivyo anajisikia vibaya kufananishwa naye japo anafurahia kuona mashabiki wanakikubali kiwango chake kwa mechi chache zilizoanza za msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kiungo huyo wa zamani wa Yanga, aliyeigomea Simba msimu uliopita kumtoa kwa mkopo kwenda kuichezea timu iliyokuja kushuka daraja ya Polisi Dodoma ameanza  msimu kwa kuonyesha kiwango cha hali ya juu akiifungia Simba mabao yaliyoiweka kileleni mwa msimamo huku mwenyewe akiongoza orodha ya wafungaji mpasa sasa.
Mchezaji huyo ameifungia Simba jumla ya mabao manne mpaka sasa, matatu akiyafunga katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Yanga waliotoka nao sare ya bao 1-1 na ile ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya JKT Oljoro, jingine alifunga walipilaza JKT Ruvu.

Mwisho

No comments:

Post a Comment