STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, October 29, 2012

Ubalozi wa UAE watoa mkono wa Idd kwa nyama ya mbuzi wa Sh Mil 40





UBALOZI wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania,  kupitia asasi yake ya Red Crescent imetumia kiasi cha Dola za Kimarekani 27,000 ambazo ni zaidi ya Sh Milioni 40 kwa ajili ya kununua Mbuzi waliochinjwa na kugaiwa waumini wa Kiislam wa mikoa minne kama 'mkono wa Idd'.
Nyama hiyo ya mbuzi iligaiwa kwa waumini wa misikiti ya wilaya zote za Dar es Salaam ambapo mkoa huo pekee walichinjwa mbuzi 250, wilaya nyingine ni Same-Kilimanjaro, Mafia-Pwani na Lushoto -Tanga.
Akizungumza kwa niaba ya Balozi wa UAE nchini Tanzania, Mallalla Mubarak Al Ameir na msaidizi wake, Mohammed Obaid Salem AlZaabi, baada ya ugawaji wa jijini Dar, Mhasibu wa ubalozi huo, Abdallah Ahmedina, alisema mgao huo ni sehemu ya taratibu za ubalozi wao kila wakati wa sikukuu za Idd.
Mhasibu huyo, alisema ni kawaida kwa ubalozi wao kila mwaka kutoa sadaka hiyo kwa waumini wa kiislam kwa nia ya kuwafariji na kuifurahia sikukuu hiyo iliyosherehekewa mwishoni mwa wiki duniani kote.
Aliongeza kwa kuwaomba waislam na wtu wengine wenye uwezo kujenga utamaduni wa kuwasaidia wasiojiweza kila mara hili kusaidia kujenga upendo na furaha baina yao.
"Ni jambo zuri kama asasi na watu wengine wenye uwezo kufanya mazoea ya kuwakumbuka watu wa kipato cha duni kwa kuwasaidia kwa hali na mali kwani hujenga upendo na furaha kwao na familia zao," alisema.
Alisema mbali na ugawaji wa nyama, pia ubalozi wao umekuwa ukiwalisha futari waumini kipindi cha mwezi wa Ramadhani pamoja na kuwapa zakatul fitri kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Eid el Fitr ya kila mwaka.

Mwisho

No comments:

Post a Comment