STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, February 24, 2013

Sheikh auwawa Zenji, ni muendelezo wa mauaji wa viongozi wa kidini


IGP Said Mwema wakati wa mkutano na waandishi wa habari kufuatia tukio la kuuwawa kwa Padri wa Kikatoliki
SIKU chache baada ya kutokea kifo cha Padri Evarist Gabriel Mushi kupigwa risasi na watu wasiojulikana kichwani eneo la Beit el Raas, Jana Imamu wa Msikiti wa Mwakaje ameuawa baada ya kupigwa mapanga hadi kufa.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ahmada Khamis amethibitisha kutokea kwa tukio hilo hapo jana mchana majira ya saa 8 na kumtaja aliyefariki kuwa ni Sheikh Ali Khamis ambaye ameuawa na watu wasiojulikana.
Kamanda Ahmada alisema Sheikh Khamis mbali ya kuwa ni Imamu wa Msikiti lakini pia ni mkulima na ameuliwa wakati akiwa katika mazingira ya kazi zake ndani ya shamba lake huko Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Akielezea mazingira ya tukio hilo Kamanda Ahmada alisema tukio hilo limetokea baada ya Sheikh Khamis kwenda shambani kwake katika shmba la minazi Kidoti ambapo wakati akiwa shambani hapo ndipo walipotokea watu kadhaa na kumpiga mapanga sehemu za shingoni mwake na kusababisha kifo chake muda mfupi baada ya kipigo hicho.
Alisema baada ya tukio hilo, watu walimchukua na kumkimbiza hospitali lakini kutokana na kupoteza damu nyingi alifariki dunia wakati akiwa njiani na hivyo harakati za mazishi zinafanyika baada ya kuchukuliwa vipimo na wataalamu wa afya.
Kamanda Ahmada ametoa wito kwa wananchi kutopuuzia taarifa za watu ambao wanawashuku na wenye kuleta maafa yakiwemo mauaji hapa nchini, kwani kuwaficha wahalifu ni kuendeleza utamaduni usiofaa katika jamii ambayo imeanza kuharibika kutokana na mauaji hayo yanayoendelea kila kukicha.
Hili ni tukio la nne kwa viongozi wa dini kuhujumiwa ambapo tukio la kwanza Sheikh Fadhil Suleiman Soraga kumwagiwa tindi kali na watu wasiojulikana na kujeruhiwa vibaya wakati akifanya mazoezi nyakati za asubuhi karibu na nyumbani kwake Magomeni, tukio la pili ni lile la Padri Ambrose Mkenda aliyepigwa mapanga shingoni na kurejuhiwa vibaya na watu wasiojulikana wakati akitaka kuingia nyumbani kwake huko Tomondo Mjini Unguja. matukio hayo mawili yalitokea mwaka jana.
Katika mwaka huu nako kumetokea matukio mawili kwa kuuawa kwa Pardi Evarist Mushi huko Beit El Raas wakati akitaka kuingia Kanisani na pia kuuawa kwa Sheikh Ali Khamis huko Kidoti shambani kwake Mkoa wa Kaskanizini Unguja.  Inna lillahi wainna ilayhi rajiiun.

No comments:

Post a Comment