STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 2, 2013

Toto African yaapa kufa na Prisons kesho Kirumba


Kocha wa Toto Africans, John Tegete (kushoto) akiwa na mwanae, Jerry Tegete
 
Kikosi cha Toto African
BAADA ya kuwabana mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba na kutoka nao sare ya mabao 2-2, kikosi cha Toto Africans ya Mwanza kimeapa kuwa kesho ni kufa au kupona itakapoikabili Prisons-Mbeya.
Toto itaikaribisha Prisons kwenye uwanja wa CCM Kirumba-Mwanza katika pambano pekee la Ligi Kuu kwa wiki hii huku wakiwa mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo licha ya sare hiyo ya juzi dhidi ya Simba.
Benchi la ufundi la timu hiyo, limesema kuwa pambano lao la kesho dhidi ya Prisons ni kama 'vita' kwa sababu wanahitaji ushindi kuweza kujiokoa kwenye janga la kushuka daraja.
Kocha Mkuu wa timu hiyo John Tegete, aliiambia MICHARAZO kwa njia ya simu toka Mwanza kwamba wamejiandaa kuhakikisha wanazoa pointi tatu katika mechi ya kesho ili kujinasua mkiani wakati wanasubiri mechi zao zilizosalia.
Tegete, alisema benchi lao limejiwekea malengo la kuhakikisha wanashinda mechi zao zote zilizosalia ili kuibakisha Toto katika Ligi Kuu.
Toto iliyopo mkiani kwa sasa ikiwa na pointi 18 sawa na Polisi Moro lakini ikizidiwa na maafande hao mabao ya kufunga na kufungwa mara baada ya mchezo huo wa kesho itakuwa imesaliwa na michezo mitatu.
Michezo hiyo ni dhidi ya wakata miwa wa Mtibwa Sugar na Kagera Sugar ambayo Toto itazifuata timu hizo, kabla ya kurejea Mwanza kumaliza msimu kwa kuvaana na Ruvu Shooting mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment