STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 2, 2013

PSG, Barca leo kimbembe Ulaya

Nyota wa Barcelona, Lionel Messi, akishangilia moja ya mabao aliyowatungua Ac Milan

David Beckham wa PSG
PARIS, Ufaransa
MPANGO wa klabu ya Paris St Germain inayomilikiwa na bilionea wa Qatar kutaka kuwa miongoni mwa timu tishio barani Ulaya utakabiliwa na mtihani mgumu leo wakati watakapowakaribisha Barcelona katika mechi yao ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Barcelona, wakitoka kujirekebisha kwa ushindi mnono wa jumla ya mabao 4-2 dhidi ya AC Milan kufuatia kipigo cha awali cha 2-0 katika hatua ya 16-bora ya michuano hiyo, wanapewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo kwa mara ya nne katika misimu nane kwenye fainali itakayochezwa Mei kwenye Uwanja wa  Wembley.
Hata hivyo, PSG waliowang'oa Valencia katika hatua ya 16-bora, wanaamini kwamba huu ndiyo wakati mzuri kwao kupata heshima ya kuwa miongoni mwa vigogo wa Ulaya.
Klabu hiyo tajiri ya Ufaransa, ikiwa chini ya kocha Carlo Ancelotti, inaelekea pia kutwaa taji lake la kwanza la Ligi Kuu ya Ufaransa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 18 na pia imetinga hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya kutookana kwa kipindi hicho.
Vinara hao wa msimamo wa Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa wamewekewa malengo magumu ya kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya katika kipindi cha miaka mitano baada ya kununuliwa na bilionea wa Qatar mwaka jana na kumwagiwa fedha nyingi kwa nia ya kujenga timu tishio barani Ulaya.
Beki wa kati, Thiago Silva, washambuliaji Zlatan Ibrahimovic na Ezequiel Lavezzi, ambao wote walisajiliwa mwaka jana, wamekuwa mhimili katika kuisaidia PSG kufika hatua ya sasa.
Mara ya mwisho wakati PSG walipofika robo fainali ya klabu bingwa Ulaya mwaka 1995, waliifunga Barcelona lakini kuna mabadiliko makubwa tangu wakati huo. PSG wamekuwa wakikosekana katika ligi ya Ulaya tangu wakati huo huku Barcelona wakitwaa ubingwa mara tatu.
Thiago Silva anaielezea mechi ya leo kwa kusema "ni mechi ambayo wote tulikuwa tukiiota" na nyota hao watatu waliosajiliwa kwa bei mbaya watalazimika kuonyesha kiwango chao cha juu leo ikiwa watataka PSG iwe na nafasi ya kushinda.
Nyota mpya wa PSG, David Beckham, aliyesajiliwa Januari kwa mkataba wa miezi mitano, anaamini kwamba wanaweza kufanya vizuri.
"Klabu hii ina malengo makubwa. Tunataka kufika mbali kadri inavyowezekana katika kila michuano," nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa.
"Ni wazi kwamba itakuwa mechi ngumu, lakini vilevile itakuwa ya kuvutia sana," aliongeza Beckham.
Matumaini ya PSG yaliongezeka baada ya Ibrahimovic kuruhusiwa kucheza dhidi ya timu yake ya zamani ya Barca baada ya kupunguziwa adhabu ya kufungiwa mechi mbili kufuatia kadi nyekundu aliyopata katika mechi dhidi ya Valencia.
Ibrahimovic alikuwa na kipindi kigumu cha mwaka mmoja wa kuichezea Barca lakini alisema kuwa kucheza tena dhidi yao leo hakutamuathiri kwa namna yoyote ile.
"Tayari nimeshacheza dhidi ya Barcelona na mechi hii (ya leo) itakuwa maalum kwa kila mmoja hapa PSG," alisema Ibrahimovic, aliyewahi kucheza dhidi ya Barca katika hatua ya makundi wakati alipokuwa AC Milan mwaka 2011.
"Namna gani ya kuwafunga ndiyo swali la kujiuliza. Tutalazimika kuwa makini na kocha pengine atatupa mbinu maalum za kuizuia timu bora zaidi duniani."
Wakati PSG wakitegemea mbinu za Ancelotti, kocha wa Barcelona,Tito Vilanova anatarajiwa kurejea kazini kwa mara ya kwanza baada ya miezi miwili ya kuwa New York alikokwenda kutibiwa kansa ya koo na nafasi yake kushikwa kwa muda na msaidizi wake, Jordi Roura.
Vilanova alirejea Barcelona wiki iliyopita na kushiriki mazoezi Ijumaa lakini hakusafiri na timu yake katika mechi yao ya ugenini dhidi ya Vigo Jumamosi.
"Kurejea kwa Tito kumeleta nguvu mpya kwa timu nzima," kipa Jose Manuel Pinto alisema baada ya sare yao ya 2-2 dhidi ya Celta Vigo.
Vilanova amewajumuisha kikosini Jordi Alba na Xavi, ambao walikosa mechi ya Jumamosi lakini sasa wote wako 'fiti' baada ya kupona maumivu ya misuli ya paja wakati walipokuwa wakiitumikia timu yao ya taifa ya Hispania.
Nahodha Carles Puyol na Adriano Correia wameachwa kutokana na majeraha, na baada ya Pedro kukosekana katika mechi ya leo kwa sababu ya kutumikia adhabu, yosso Cristian Tello anaweza kuanza kikosini.

Vikosi vinavyotarajiwa leo:
Paris St Germain: Salvatore Sirigu; Christophe Jallet, Thiago Silva, Alex, Maxwell; Lucas, Marco Verratti, Blaise Matuidi, Javier Pastore; Zlatan Ibrahimovic na Ezequiel Lavezzi
Barcelona: Victor Valdes; Dani Alves,Gerard Pique, Javier Mascherano, Jordi Alba; Sergio Busquets, Xavi, Andres Iniesta; Cesc Fabregas, Lionel Messi na David Villa.

No comments:

Post a Comment