STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, July 13, 2013

Bint Mfalme wa Saudia akamatwa kwa unyanyasaji

 
MWANAMKE mmoja anayetajwa kuwa Binti wa Mfalme wa Saudi Arabia, Meshael Alayban, 42, amekamatwa katika jimbo la Carlifonia nchini Marekani na kutuhumiwa kuhusika na biashara ya watu.
Bi Alayban anakabiliwa na mashtaka ya kumlazimisha mama mmoja kutoka Kenya kufanya kazi kwa zaidi ya saa kumi na sita kila siku, na kumlipa kiasi kidogo cha pesa kuliko walivyokuwa wameafikiana.
Utawala wa eneo hilo, umesema kuwa bint mfalme huyo alichukua pasi ya kusafiria ya mama huyo, hatua iliyomfanya atoroke.
Mawakili wa mtuhumiwa huyo wametaja kesi hiyo kuwa mzozo kuhusu hali ya utendaji kazi.
Novemba mwaka uliopita, wapiga kura katika jimbo la Carlifonia, waliidhinisha sheria kali dhidi ya watu watakaopatikana na hatia ya kuhusika na ulanguzi wa watu.
Ikiwa atapatikana na hatia, Bi Alayban, huenda akahukumiwa kifungo cha miaka kumi na miwili gerezani, adhabu ambayo ni asilimia mia moja zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya wapiga kura kuidhinisha mageuzi sheria hiyo mpya.
Waendesha mashtaka wanasema Bi Alayban, ni mmoja wa wake sita wa Mwana Mfalme Abdulrahman bin Nasser bin Abdulaziz al-Saud, mmoja wa wanawe wa kiume wa familia moja ya kifalme nchini Saudi Arabia.

Mama huyo kutoka Kenya ambaye jina lake halijatolewa, aliajiriwa na Bi Alayban miaka miwili iliyopita, baada ya kusaini mkataba na shirika moja la kutoa uajiri nchini Saudia.
Mkenya huyo aliahidiwa kulipwa dola 1,600 kila mwezi na kuwa atafanya kazi kwa saa nane kila siku kwa siku tano.
Hata hivyo, Bi Alayban amekuwa akimlipa dola 220 kwa  mwezi na kulazimishwa kufanya kazi kwa zaidi ya saa 16 kila siku.
Mama huyo amedai, kupokonywa pasi yake ya kusafiria na alikabidhiwa muda mfupi tu kabla ya wao kusafiri kwenda Carlifonia na Bi Alayban.
Akiwa Carlifonia, alilazimishwa kufanya majukumu mengi zaidi ya nyumbani kwa familia ya watu wanane waliokuwa katika vyumba vinne tofauti, ambako amedai alizuiliwa mateka.
Wakati alifanikiwa kutoroka, alisimamisha basi moja na kwenda moja kwa moja hadi kituo cha polisi.
Bi Alayban alikamatwa siku ya Jumatano na kufikishwa mahakamani juzi Alhamisi.
Aliachiliwa huru kwa dhamani ya dola milioni tano na kuamriwa kurejesha pasi ya kusafiria ya amama huyo kutoka Kenya.
Aidha Bi Alayban sasa atavalia chombo maalum ambacho kitatoa maelezo ya mahala aliko na hataruhusiwa kuondoka Marekani hadi kesi hiyo itakapokamilika.
Viongozi wa Mashtaka walitaka jaji kumuachilia kwa dhamani ya dola milioni 20 au anyimwe dhamana kwa kuwa yeye ni tajiri mkubwa na aweza kutoweka.

No comments:

Post a Comment