Hussein Javu akiwa katika pozi |
Javu alisema hata taarifa kwamba amesajiliwa Yanga kwa mkataba wa miaka mitatu anazisikia tu hewani, ila ukweli suala hilo sio kweli kwa vile hajasaini mkataba wowote na mabingwa hao wa soka nchini.
Akizungumza na MICHARAZO, mshambuliaji huyo aliyekuwa kinara wa mabao ndani ya Mtibwa Sugar na mmoja wa wachezaji wanaounda timu ya pili ya taifa 'Young Taifa Stars' alisema Simba na Yanga kwa nyakati tofauti walimfuata kwa nia ya kumshawishi kujiunga na timu zao, lakini aliwaelekeza wamalizane na 'mabosi' wake.
"Unajua mimi bado nina mkataba na Mtibwa, pia klabu hii nimetoka nayo mbali hivyo sikuwa na maamuzi zaidi ya kuwataka Simba na Yanga wazungumze na uongozi wa klabu yangu na kwa msingi huo yaliyoendelea au yanayoendelea siyajui," alisema.
Kuhusu kwamba tayari keshasaini mkataba wa miaka mitatu Yanga, Javu alisema hilo halina ukweli kwa sababu hakuna fomu zozote alizosaini mpaka sasa na kushangaa habari hizo kusambazwa kwenye vyombo vya habari.
"Ningekuwa nimesaini ndugu yangu ningekuambia ukweli, hilo halijafanyika na wala sijajua kinachoendelea au kujua kama msimu ujao nitacheza Mtibwa, Yanga au Simba," alisema.
Aliongeza kuwa, yeye kama mchezaji anasubiri kusikia maelekezo ya viongozi wake kama wameafikiana na Yanga au Simba na wangetaka kumuuza hatakuwa na tatizo na kama wataamua kumbakisha Mtibwa Sugar kwa msimu mwingine pia kwake ni sawa tu kwani anafurahia maisha katika klabu hiyo ya Manungu.
"Nikibakishwa Mtibwa Sugar au kuuzwa Yanga au Simba poa mradi masilahi yawepo kwani soka ndiyo ajira yangu na siwezi kuchagua mahali pa kwenda," alisema.
Dai la kwamba yeye ni majeruhi wa kudumu wa goti, Javu alisema taarifa hizi zinalengo la kumharibia kwani hajawahi kuumia kwa siku za karibuni na kushangaa wanaompakazia uzushi huo.
Alisema anadhani wanaomzushia wanafanya hivyo kwa minajili ya kukomoana baina ya Simba na Yanga ambao wamekuwa na mvutano wa kumwania mara baada ya ligi kuu msimu uliopita kumalizika.
No comments:
Post a Comment