STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Sunday, October 13, 2013

Drogba aibeba Ivory Coast, waifyatua Senegal 3-1 WCQ

drog
MSHAMBULIAJI nyota wa timu ya taifa Ivory Coast, Didier Drogba alirejea kwa kishindo katika timu hiyo baada ya kuiongoza kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Senegal katika pambano la kwanza la mtoano wa kuwania nafasi tano za kutinga Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.
Drogba aliitwa tena katika kikosi hicho baada ya awali kuwekwa kando na kusaidia kufunga bao la penati kabla ya Solomon Kalou kufunga la tatu huku la pili wageni wao wakijifunga wenyewe.
Ivory Coast 'The Elephants' sasa imeingia mguu mmoja ndani kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia ikihitaji sare yoyote katika mechi ya marudiano baadaye kukihakikisha kucheza fainali hizo kubwa duniani.
Mlinzi wa Senegal Ludovic Sane aliizawadia wenyeji bao kabla ya Kalou kufunga bao la tatu na dakika za lala salama Papiss Demba Cisse aliifungia Senegal bao la kufutia machozi ambalo linaweza kuwa msaada kama Senegal itaenda kushinda nyumbani mabao 2-0 katika mechi ya marudiano. Katika pambano jingine Burkina Faso wakiwa kwenye uwanja wao wa Agosti 4 waliwafunga Algeria 3-2 katika mchezo uliokuwa na upinzani wa aina yake .
Mabao ya Burkinabe yalifungwa na Jonathan Pitroipa , Aristide Bance na Djakaridja Kone huku Algeria wakifunga kupitia kwa Soufiane Feghouli na Carl Medjani. Bukinabe sasa wanahitaji sare yoyote katika mechi ya marudiano itakayofanyika ugenini kufuzu fainali hizo ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwao.
Michezo hiyo ya kuwania fainali hizo za Kombe la Dunia hatua ya mwisho kwa nchi za Afrika zitaendelea tena leo kwa mabingwa wa Afrika Nigeria kuwa ugenini mjini Addis Ababa kupepetana na wenyeji wao Ethiopia, wawakilishi pekee wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) huku timu iliyopenya baada ya Cape Verde kuenguliwa kwa udanganyifu Tunisia itaialika Cameroon na keshokutwa Jumanne Ghana watakuwa wenyeji wa Misri.

No comments:

Post a Comment