STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Thursday, October 10, 2013

Kibadeni kupasua la rohoni kesho Msimbazi


Kocha wa Simba  Abdallah Kibadeni akiwa kwenye mazoezi ya timu hiyo
KOCHA Mkuu wa klabu ya Simba, Abdallah Kibadeni kesho anatarajiwa kuteta na wanahabari kuweka mambo sawa juu ya kinachoendelea katika kambi ya klabu yake pamoja na maandalizi yao dhidi ya mchezo wao na Prisons-Mbeya utakaochezwa Jumamosi kwenye uwanja wa Taifa.
Akizungumza na MICHARAZO, Kibadeni alisema amelazimika kuitisha mkutano huo kutokana na baadhi ya magazeti kuripoti taarifa 'mbaya' dhidi ya kambi yake na benchi nzima la Simba kitu alichodai kinachafua taswira ya Simba na kuleta sintofahamu miongoni mwa wanachama na mashabiki wao.
Kibadeni aliyeichukua timu hiyo baada ya Mfaransa Patric Liewig kutimuliwa alisema mkutano huo utafanyika majira ya saa 5 asubuhi ya kesho kwenye makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi.
"Kuna baadhi ya wanahabari wamekuwa wakituchonganisha Simba, hivyo nimeitisha mkutano kesho nizungumze kuweka mambo sawa, kadhalika kuelezea maandalizi ya jumla dhidi ya pambano leo na Prisons," alisema Kibadeni maarufu kama King Mputa.
Kibadeni aliongeza kuwa, kuanza sasa wanahabari watakaotaka kujua chochote kuhusu Simba ni lazima wapate taarifa hizo kwa Msemaji wa Klabu, Ezekiel Kamwaga hata yale ya ufundi ambapo atakuwa anawauliza benchi la ufundi na kutoa majibu kwa wanahabari ili kuhofia kuivuruga Simba inayoongoza Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 15.
Naye Msemaji wa Simba, Kamwaga alithibitisha kuwepo kwa mkutano huo wa kesho, akidai kocha wao hajafurahia na baadhi ya taarifa zinazoripotiwa zinazoonekana kama zina lengo la kuivuruga timu yao.

No comments:

Post a Comment