STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, October 16, 2013

Mazito yaibuka kupigwa risasi kwa Ufoo Saro


MAZITO yameibuka kufuatia kupigwa risasi kwa Mtangazaji wa Independent Television (ITV), Ufoo Saro na mtu anayedaiwa ni mzazi mwenzake, Ateri Mushi, Risasi Mchanganyiko lina mkanda mzima.
Ufoo Saro akitolewa chumba cha upasuaji.
Ufoo alipigwa risasi na mwanaume huyo na kujeruhiwa tumboni na mguuni katika tukio lililotokea Oktoba 13, mwaka huu nyumbani kwa mama yake mzazi, Anastazia Saro, Kibamba, Dar es Salaam kufuatia kutoelewana kati ya wawili hao.
Katika tukio hilo la kutisha, Ateri pia alimuua kwa risasi mama wa Ufoo na kujiua mwenyewe na maiti zao kupelekwa Muhimbili.

MAZITO YALIYOIBUKA
Juzi, Shekilango, Ubungo jijini Dar, Risasi Mchanganyiko lilizungumza na rafiki mmoja wa marehemu Ateri aliyejitambulisha kwa jina moja la Urassa ambaye aliweka wazi mambo anayoyajua kuhusu marehemu kabla ya kujiua kwa risasi.
Alisema tangu mwaka huu (2013) uanze, marehemu Ateri alikuwa akilalamika kwamba, anampenda sana Ufoo lakini hamuelewielewi.


“Tangu mwaka huu ulipoanza nimekuwa nikiwasiliana na Ateri. Alikuwa akisema anampenda sana Ufoo lakini kama hamuelewielewi katika mambo fulani ya uhusiano.
“Alisema kukaa kwake mbali (Sudan) na mchumba wake huyo anahisi kama mambo yanakwenda kufikia mwisho wa uchumba wao. Kwa jumla Ateri alishajua nini atakifanya mwaka huu kuhusu uhusiano wake na yule mtangazaji maana maneno yake mengi yalikuwa ni malalamiko tu,” alisema Urassa.

MAREHEMU ALISEMA AMECHOKA KUISHI
Akienda mbele zaidi, Urassa alisema Septemba, mwaka huu marehemu alimpigia simu na kumwambia anahisi amechoka kuishi kwenye dunia hii yenye maumivu ya mapenzi kila kukicha.
“Nilimuuliza amechoka kuishi kivipi? Akanijibu anaona kuna mambo hayaendi sawa kama anavyotaka yeye kwa huyo mchumba wake. Lakini kwenye simu hakuniambia kama hayo mambo ni yapi? Ila nahisi ni mapenzi yao,” Urassa alizidi kutoboa.
 
Ufoo Saro.
ALIIBUA TABIA YA KUPENDA KUSALI
Katika mazungumzo na Urassa, pia alimgusia marehemu kwamba kwa siku za karibuni aliibua tabia ya kusali kila wakati kuliko siku za nyuma.
“Siku moja akiwa Sudan alinipigia simu, akasema anapenda kama mahali anapoishi kule pangekuwa na kanisa karibu ili awe anasali alfajiri, mchana na jioni lakini akaniambia kule hakuna makanisa.
“Nilimuuliza mbona amepanga kusali mara tatu zote hizo kwa siku, akanijibu binadamu tunatakiwa kujiandaa kwani saa yoyote roho inaweza kutoka,” alisema Urassa.

Baadhi ya wananchi na wanahabari wakiwa hospitalini kujua hali ya Ufoo.
MAREHEMU ALIKUWA AKILIA WIVU
Risasi Mchanganyiko: Kwa hiyo unawaza nini kuhusu marehemu kumuua mama mkwe wake na kumjeruhi mchumba wake kisha na yeye kujimaliza?
Urassa: Kwa kweli ninavyojua mimi ni wivu tu. Unajua yule alikuwa yuko kikazi Sudan, mchumba wake yupo Dar. Mfano siku moja aliniambia anatamani apate mtu wa kumfuatilia Ufoo kwenye nyendo zake za kila siku kwani anahisi anaibiwa japo hakuniambia kama ana uhakika.
DALILI ZA MAUAJI ZILIONEKANA MAPEMA
Kwa mujibu wa ndugu, licha ya kwamba hawakujua litakalotokea mbele, lakini baada ya kutokea ndiyo wamebaini kwamba marehemu Mushi alishabadilika roho muda mrefu.
Walisema uchangamfu na utani aliokuwa nao siku za nyuma alipokuwa akienda kuwatambelea viliisha ghafla kwani hivi karibuni alikuwa akienda, baada ya salamu hakuwa akiongeza neno.

LENGO LA MAREHEMU
Kwa mujibu wa watu waliofika nyumbani kwa mama Ufoo mapema, marehemu alionesha dalili za kuteketeza familia hiyo.
“Huyu bwana (marehemu) nahisi alitaka kutekeza familia, maana kabla ya kujiua yeye, alipiga risasi mtungi wa gesi ukiwa na nguo, ukalipuka. Sasa hapo unadhani lengo lake lilikuwa nini kama si kuiangamiza familia yote ya mzee Peter Saro?” alisema jirani mmoja kwa mtindo wa kuhoji.

UFOO ALILIJUA HILO
Habari zinasema baada ya Ufoo kupigwa risasi, akiwa anatambaa na damu zake tumboni aliwataka ndugu zake kutotoka kwani shemeji yao alikusudia kuwaua wote. Kauli ya Ufoo inakwenda sambamba na madai ya mzee aliyesema dhamira ilikuwa kuiangamiza familia hiyo.

ALIKUWA HAELEWANI NA BABA WA UFOO
Godluck Saro ni mdogo wa Ufoo, yeye akizungumza na gazeti hili juzi, nyumbani kwao, Kibamba, Dar alisema marehemu shemeji yake alikuwa haelewani kabisa na baba wa Ufoo, marehemu mzee Peter Saro aliyefariki dunia Julai 16, 2011 kwa shinikizo la damu.
“Kwanza shemeji alianza kufika hapa nyumbani baada ya baba kufariki, kabla ya hapo alikuwa hafiki maana walikuwa hawaelewani kabisa. Baba alikuwa anasema shemeji ni mkorofi, hawezi kuwa mume wa dada,” alisema kijana huyo.  

MAJIRANI WA KWA UFOO
Juzi, Risasi Mchanganyiko lilipata bahati ya kuzungumza na baadhi ya majirani wa kwa Ufoo, Mbezi jijini Dar es Salaam ambapo karibu wote walidai kusikia majibizano ya muda mrefu usiku wa kuamkia siku ya tukio.
“Tulisikia majibizano kwa muda mrefu ule usiku, lakini si ya wazi sana kiasi cha kumfanya mtu ajue nini kilikuwa kinaongelewa,” alisema jirani mmoja.
“Mimi alfajiri wakati wanaondoka niliwasikia, lakini sikujua wanakwenda wapi na nilijua wapo na amani tu kwani hakukuwa na mazungumzo ya ugomvi,” alisema jirani mwingine.

UFOO NA MAREHEMU
Ufoo yeye bado amelazwa Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu. Yeye na marehemu walibahatika kupata mtoto mmoja wa kiume, Alvin Ateri Mushi.

MAZISHI YA WOTE
Juzi, ndugu wa marehemu Mushi walikutana katika kikao cha ratiba ya mazishi pale 92 Hotel, Shekilango - Ubungo, Dar ambapo walisema mwili wa marehemu utasafirishwa kabla ya Ijumaa kwenda kijijini kwao Uru, Moshi kwa mazishi.
Mwili wa marehemu Anastazia ulisafirishwa jana kwenda Machame, Moshi ambapo mazishi yake yalipangwa kufanyika leo katika eneo hilo.
Mwenyezi Mungu aziweke pema peponi roho za marehemu. Amina.


GPL

No comments:

Post a Comment