STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, January 7, 2014

Hivi ndivyo Waziri Mgimwa alivyozikwa mjini Iringa

Familia yake katika salamu za mwisho kabla kaburi lake halijafukiwa.
MAISHA katika uso wa dunia ya aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Dk William Mgimwa yamehitimishwa jana kijijini kwake Magunga wilayani Iringa mkoani Iringa.

Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda waliongoza watu wanaokadiriwa kuwa 10,000 kuupumzisha mwili wa Dk Mgimwa katika nyumba yake ya milele.

Pamoja na Rais na Waziri Mkuu, mawaziri mbalimbali, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, watendaji wa wizara, na viongozi wa CCM na vyama vya upinzani walihudhuria mazishi hayo.
Rais Kikwete na wasaidi wake

Akiendesha ibada ya kumuombea marehemu, Msaidizi wa Makamu wa Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki Songea, Julius Kangalawe aliomba Mungu awajalie na awape maisha marefu wanasiasa wanaohangaikia masikini.

“Siku hizi hakuna udugu, wenye nacho wanataka kuendelea kuwa nacho, watu wanaogopana, udugu umechakachuliwa na masikini wanaendelea kuwa masikini,” alisema.

Tofauti na viongozi wengi, alimsifu Dk Mgimwa kwa kuwa mnyenyekevu, mpenda watu na aliyetumia akili zake nyingi alizokuwa nazo kwa maendeleo ya watu.
 
Julius Kangalawe
“Umati huu mkubwa wa watu unadhihirisha jinsi Dk Mgimwa alivyokonga nyoyo za watu;inaonesha jinsi alivyokuwa mpenda haki, leo amepumzishwa katika nyumba yake hii, kesho hatujui nani atamfuata, lakini watakaomfuata wapo hapa hapa,” alisema.

Alimuomba Mungu awajalie watanzania wawe na siasa bora inayojali masikini kwa kuwa hiyo ndiyo njia ya kuwafananisha binadamu.
 
waombolezaji
“Leo hii wanasiasa  wanaingia katika ofisi zao baada ya kuomba Mungu kwa kutumia vitabu vitakatifu, lakini wengi wao ni waongo; wanatumia maandiko matakatifu kufanya udanganyifu, wakishakula kiapo, na vitabu vya Mungu wanatupa,” alisema.

Alisema pamoja na kiu kubwa waliyonayo watanzania ya kupata Katiba mpya, haiwezi kuwasaidia kwasababu bila Mungu hakuna linalowezekana.
 
Mwili wake ukipelekwa katika nyumba yake ya milele
“Hata katiba hiyo iwe nzuri kiasi gani, majambazi wataendelea kuwa majambazi, mafisadi vivyo hivyo na masikini wataendelea kudhulumia haki zao, kwasababu hakuna upendo wa Mungu,” alisema.

Alisema Katiba pekee inayoweza kumaliza matatizo ya watanzania ni zile sheria zilizoandikwa na Mwenyezi Mungu kwani ndizo zenye uwezo wa kubadili maisha.

Akitoa salamu za serikali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema afya ya Dk Mgimwa ilianza kuteteleka alipokuwa kikazi Marekeni mwishoni mwa mwaka jana.

“Serikali iliamua kumpeleka Afrika Kusini kwa matibabu, hata hivyo Mungu alimpenda zaidi na akayachukua maisha yake,” alisema.



Alisema Dk Mgimwa alikuwa mchapa kazi aliyeonesha muelekeo wa kuituliza serikali katika nafasi nyeti ya Waziri wa fedha.

“Serikalini tulianza kutulia, tukiamini wizara imepata mtu; kazi tuliyonayo ni kuenzi tunu alizokuwa nazo. Alikuwa mchapa kazi mwenye akili nyingi,” alisema.

Mwakilishi wa kambi ya Upinzani Bungeni, Mchungaji Peter Msigwa (MB) alisema taifa lilikuwa linamuhitaji Dk Mgimwa kwani alionesha tofauti kubwa na wazee wengine kwa kujali maendeleo ya watu.
 
“Alikuwa makini bungeni, aliacha itikadi za vyama alipokuwa akitekeleza majukumu yake, na mara kadhaa alikuwa akichukua hoja za wapinzani na kuzifanyia kazi,” Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini alisema.

Alisema binadamu hawajaumbwa ili kuleta matatizo kwa wengine na ndio maana thamani ya utu wao huhesabiwa kwa haki wanayotenda kama alivyokuwa Dk Mgimwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma alimkumba Dk Mgimwa kwa uchapi kazi wake huku akiwasilisha rambirambi ya Sh Milioni 5 kwa familia ya marehemu.

Akitoa shukrani za familia, mtoto wa Dk Mgimwa, Godfrey Mgimwa alizitaja kazi nyingi zilizkuwa zikitekelezwa na baba yake katika jimbo lake la Kalenga na kuiomba serikali kuziendeleza.

Kazi hizo ni pamoja na kusomesha watoto yatima, ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari, ujenzi wa miundombinu na mawasiliano, misaada kwa vikundi vya ujasriamali, na mkazo katika huduma za jamii ikiwemo afya, kilimo, na maji.
 
wafanyakazi wa wizara yake wakiweka mashada katika kaburi lake
Alisema siku kumi kabla ya kifo cha baba yake, alimwambia ameandaa mabati 120 anayotaka kuyagawa katika maeneo mbalimbali jimboni mwaka kwa lengo la kusukuma maendeleo.

Alimpongeza Rais Kikwete kwa upendo na ushirikiano aliotoa kwa familia yao katika kipindi chote ambacho baba yao alikuwa mgonjwa hadi kifo chake.

“Rais alionesha uzalendo na upendo wa hali ya juu kwani alimtembelea baba mara mbili akiwa amelazwa hospitalini,” alisema.

wawakilishi taasisi za fedha
Pamoja na Rais na Waziri Mkuu, mawaziri mbalimbali, wabunge, wakuu wa mikoa, watendaji wa wizara, na viongozi wa CCM walihudhuria mazishi hayo.
wakuu wa wilaya na mikoa
Joseph Mungai akiwakilisha wazee

No comments:

Post a Comment