STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, January 8, 2014

Yanga yaomba radhi, yamwaga noti Mapinduzi Cup

Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
KLABU ya Yanga SC imeomba radhi kwa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd kwa kitendo chao cha kujitoa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, sambamba na kutoa Sh. Milioni 10 kwa Kamati ya Mashindano hayo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Sanga alikutana na Balozi Seif Ali Idd ofisini kwake eneo la Vuga, karibu na Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa mazungumzo ya kuomba radhi.
Clement Sanga kushoto akiwa na Mwenyekiti wake, Yussuf Manji. Leo ametua Zanzibar kuomba radhi na kutoa Sh. Milioni 10 kwa Kamati ya Kombe la Mapinduzi 

Balozi Seif ameupokea msamaha huo na pamoja na hayo, Sanga aliahidi Yanga itakuja Zanzibar mwezi ujao kucheza mechi tatu za kirafiki na hawatachukua fedha za mapato ya milangoni, ili ziende kwenye mfuko wa Kombe la Mapinduzi.
Yanga SC ilijitoa kwenye Kombe la Mapinduzi kwa sababu haikuwa na benchi la Ufundi, baada ya kuwafukuza makocha wake wote, Mholanzi Ernie Brandts na wasaidizi wake, Freddy Felix Minziro na Mkenya Razack Ssiwa, kufuatia kufungwa na mahasimu wao wa jadi, Simba SC mabao 3-1 katika mechi ya Nani Mtani Jembe Desemba 21, mwaka jana.
Kwa sasa tayari Yanga SC imeajiri makocha wawii, Msaidizi Charles Boniface Mkwasa na kocha wa makipa Juma Nassor Pondamali, wakati mchakato wa kumsaka kocha mkuu wa kigeni unaendelea.
Msafara wa zaidi ya watu 32 wa Yanga SC unatarajiwa kuondoka kesho alfajiri kwenda Uturuki kwa kambi ya wiki mbili, kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga walitarajiwa kupata viza zao jioni ya leo na kesho watapanda ndege ya Uturuki (Turkish Airline) kwenda kwenye kambi ya mafunzo katika nchi hiyo ya Ulaya kwa mara ya pili mfululizo.  
Wachezaji wanaotarajiwa kuondoka na timu hiyo kesho ni makipa; Juma Kaseja, Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki David Luhende, Oscar Joshua, Juma Abdul, Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Job Ibrahim na Rajab Zahir.
Viungo ni Hassan Dilunga, Bakari Masoud, Hamisi Thabit, Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Nizar Khalfan, wakati washambuliaji ni Jerry Tegete, Hamisi Kiiza, Emmanuel Okwi, Mrisho Ngassa, Said Bahanuzi, Shaaban Kondo, Didier Kavumbangu, Simon Msuva, Reliant Lusajo na Hussein Javu.
Viongozi ni makocha Charles Boniface Mkwasa na Juma Pondamali, Daktari Juma Sufiani, Meneja Hafidh Saleh na Ofisa Habari, Baraka Kizuguto. 
Kunaweza kukawa na watu wengine katika msafara huo kutoka kwenye uongozi, lakini bado haijajulikana ni akina nani.
Wachezaji ambao wameachwa ni Athumani Iddi ‘Chuji’ aliyesimamishwa kwa utovu wa nidhamu, Salum Abdul Telela ambaye ni majeruhi na wachezaji waliopandishwa kutoka timu ya vijana, Issa Ngao, Yussuf Abdul na Abdallah Mguhi ‘Messi’.

No comments:

Post a Comment