STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 18, 2014

Yanga imepania, yamtuma Mkwasa Cairo kuifanyia ushushushu Al Ahly

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiyhILGXEPzcg08Ou6VWhyphenhyphenGQ_bEGVRsjHkUwM-95WMFyKgoa3AmSEp0pQFl7LDHsP8AUvz0B1SdcA1_DqHCjiLzsmNFvGJVgE7hf4UYU6HgdkrfVXUq4_nOTvCDcVKeGrucIGKzxSSwSOHl/s640/Charles-Boniface-Mkwasa1.jpg
Charles Boniface Mkwasa aliyeondoka nchini leo mchana
Yanga watakaowavaa Al Ahly ya Misri Machi mwaka huu kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika
KATIKA kuhakikisha kwamba Wamisri hawaponi kwa vijana wa Jangwani, Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa 'Master' ameondoka nchini mchana wa leo kuelekea Cairo nchini Misri ili kwenda kuipeleleza Al Ahly katika mechi yake ya fainali ya Super Cup dhidi ya Cs Sfaxien ya Tunisia.
Mechi hiyo itachezwa Alhamisi na Mkwasa ataenda kuwafanyia ushushushu Al Ahly watakaovaana nao kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mapema mwezi ujao.
Kwa mujibu wa tovuti ya klabu Yanga, imesema kuwa Mkwasa ataenda kushuhudia mchezo huo Super Cup inayozikutanisha Bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika na wale wa Kombe la Shirikisho Afrika, mchezo utakaochezwa katika dimba la Cairo International Stadium.
Mkwasa ameondoka kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Ethiopia Airline ambapo atapitia jijini Adis Ababa kabla ya kuunganisha kuelekea Cairo ambapo atatua Uwanja wa Ndege majira ya saa 7 usiku na kupokelewa na wenyeji kutoka ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Misri.
Kutokana na umuhimu wa mchezo huo Uongozi wa Young Africans kwa pamoja na Benchi la Ufundi walikaa na kukubaliana kuwa kocha msaidizi Mkwasa aende kushuhudia mchezo huo wa fainali ambao utaweza kusaidia kupata picha ya wapinzani Al Ahly ambao watacheza na Young Africans mwishoni mwa mwezi huu.
Lengo la safari ni kuweza kuwaona Al Ahly wanavyocheza katika mchezo huo wa fainali, pili ni kujua wanayocheza wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani na tatu ni kuijua timu nzima kiufundi inachezaje.
Kwa upande wake Kocha Mkwasa amesema anaamini ataitumia vizuri nafasi hiyo ya kuutazama mchezo wa Super Cup kwa kuwasoma wapinzani na pindi atakaporejea atasaidiana na kocha mkuu kuwaandaa vijana tayari kwa mchezo huo.
Mkwasa mara baada ya kuutazama mchezo huo dhidi ya CS SFaxien siku ya Alhamis jioni saa 11 kamili kwa saa za Afrika Mashariki atarejea nchini siku ya ijumaa n akuungana na kikosi kwa ajili ya mchezo wa siku ya jumamosi dhidi ya timu ya Ruvu Shooting.
Al Ahly Mabingwa watetezi wa klabu Bingwa Barani Afrika watacheza na Young Africans Tarehe 1 Machi 2014 katika mchezo wa kwanza wa kuwania kuingia katika 16 bora kisha kurudiana jijini Cairo wiki moja baadae.
Rekodi inaonyesha kuwa Yanga haijawahi kuifunga achilia mbali kuitoa timu yoyote ya Afrika Kaskazini katika michuano ya kimataifa na safari hii wana jangwani wameapa ni lazima mzizi wa futina ukatwe kwa kuwaondosha na kuwavua taji Al Ahly katika mechi zao za raundi ya kwanza.

No comments:

Post a Comment