STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, February 18, 2014

16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya haponi mtu!

* Man City vs Barca, kesho Arsenal v Bayern Munich
Manchester City watakaoikuwa nyumbani

'Mnyama' Lionel Messi atafanya nini Etihad kuisaidia Barca?

Tegemeo la Arsenal Mesut Ozil kesho ataibeba vipi the Gunners

VITA tupu Ulaya leo na kesho! Ndivyo unavyoweza kusema wakati  hatua ya mtoano ya 16 Bora inapoanza leo na kuendelea kesho kwenye Ligi yua Mabingwa Ulaya.
Vinara wa mabao wa England, Manchester City watakabiliwa na wakati mgumu watakapovaana na miamba ya daraja la juu barani Ulaya, Barcelona kwenye dimba lake la nyumbani la Etihad.
Mechi hiyo ya kukata na shoka inaelezwa kuwa ya kihistoria kutokana na timu zote kushinda kwa kishindo michezo yao ya mwisho Jumamosi, ambako City ilirejea katika kiwango chake cha juu na kuifunga Chelsea 2-0 kwenye Kombe la FA wakati Barcelona yenyewe ikiisambaratisha Rayo Vallecano  kwa mabao 6-0 kwenye La Liga.
Timu zote pia zimeongezewa nguvu baada ya wachezaji wao majeruhi kurejea. Samir Nasri amerudi kikosini katika kipindi cha pili akitokea benchi baada ya kukosa mechi saba na kufunga bao moja katika ushindi wa 2-0 waliopita dhidi ya Chelsea.
Kwa upande wa Barca, Neymar naye aliingia akitokea benchi na kisha kufunga ukurasa wa mabao kwa miamba hiyo ya Nou Camp wakati ikiibuka na ushindi wa 6-0.
Neymar anatarajiwa kuanzia benchi leo jambo ambalo litatoa ahueni kwa City, ambayo itapandisha juu kiwango chao cha soka kama itawatoa mabingwa hao mara nne wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kocha wa City, Manuel Pellegrini yupo makini na anatambua ubora wa Barca kutokana na kipindi chake akiinoa Villarreal, Malaga na Real Madrid huko Hispania, pia kiungo wa City, Yaya Toure kipindi chake cha miaka mitatu alichocheza Nou Camp na kushinda kila kombe kubwa, ikiwa ni pamoja la Ligi ya Mabingwa Ulaya 2009 anaifahamu ndani nje.
Katika mahojiano na Jarida la Champions, Toure alisema ninatarajia City itashinda mechi yake ya kwanza ya mtoano ili kuonyesha ni kwa kiasi gani klabu imepiga hatua tangu Sheikh Mansour aanze kuwekeza fedha akitaka kuibadilisha kutoka uwezo wa michuano ya ndani kwenda Ligi ya Mabingwa Ulaya.
"Mashabiki wetu wanastahili ushindi dhidi ya klabu kubwa ili kuonyesha ni kwa kiasi gani klabu inaendelea," alisema. "Barcelona ni mfano sahihi, ni klabu kubwa yenye historia ya kipekee ambayo kwa sasa ina wachezaji bora duniani kama Lionel Messi, Iniesta, Xavi, Pique, Busquets.
"Itakuwa mechi kubwa na ni wazi tunatamani kuonyesha City ipo katika njia sahihi."
City haina jina katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwani imetolewa mara mbili katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika awamui mbili ilizoshiriki hivi karibuni.
Lakini msimu huu ndiyo timu inayoongoza kwa kupachika mabao kwenye michuano hiyo baada ya kufumania nyavu mara 28.
"Uzoefu wetu tulioupata kutokana na kipigo msimu uliopita umetufanya kupevuka zaidi mwaka huu," Toure aliongeza.
"Tunao wachezaji, kocha, lakini pia unapaswa kucheza na timu kubwa ili kujaribu kiwango cha uwezo wako."
City iliishangaza Bayern Munich kwa kuichapa mabao 3-2 ugenini katika hatua za makundi na imefunga jumla ya mabao 117 katika mashindano yote msimu huu.
Lionel Messi, ambaye amerejea uwanjani Januari mwaka huu baada ya kuwa majeruhi kwa miezi miwili, alifunga mabao mawili na kumpiku Alfredo di Stefano katika historia ya ufungaji La Liga.
Messi amefumania nyavu mara  228 katika mechi 263 alizocheza ambazo zinamfanya kujiunga nafasi ya tatu sambamba na Raul, wakiwa nyuma ya Telmo Zarra (251) na Hugo Sanchez (234).
Messi hadi sasa ameifungia Barcelona jumla ya mabao 337 katika michuano yote, hivyo kuweka rekodi katika klabu hiyo, lakini amefanikiwa kufunga bao moja tu nchini England wakati wa mechi ya fainali kati ya Barcelona na Manchester United iliyopigwa Uwanja wa Wembley 2011.
Licha ya Messi kuwa katika kiwango cha juu Jumamosi, pia  kiungo Cesc Fabregas na Andres Iniesta walicheza vizuri huku Pedro na Alexis nao wakifunga wakati Barca akichanua dhidi ya Rayo katika Uwanja wa Nou Camp.
"Ushindi utatusaidia kujiamini katika mechi inayofuata, ambayo itakuwa ngumu sana,"  Pedro alisema.
"Tumekuwa katika kiwango bora msimu huu, lakini leo ni kimoja kati ya bora," aliongeza nyota huyo wa Kimataifa wa Hispania.
"Mechi ya Jumanne (leo) dhidi ya City itakuwa ya karibu kuipigania, wote tu timu bora."
Mbali na mechi hiyo, leo pia
Bayer Leverkusen itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Paris St Germain  ambayo itakuwa ikimtegemea mkali wao Zlatan Ibrahimovic huku kesho Arsenal ikiialika Bayern Munich Emirates na AC Milan ikiwa mwenyeji wa Atletico Madrid.

No comments:

Post a Comment