MKURUGENZI
wa Kampuni ya Lino International Agency, Hashim Lundenga, amekanusha
uvumi uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii mapema jana usiku, kuwa
Sitti Abbas Mtemvu (pichani katikati) amelazimika kuvua taji la Urembo
la Tanzania (Redd’s Miss Tanzania 2014).
Uvumi
wa Sitti kuvua taji hilo umetokana na taarifa zilizotolewa kupitia
akaunti ya Facebook mrembo huyo anayelalamikiwa kughushi vyeti vya
kuzaliwa, akisema kutokana na vidole vya lawama anavyonyooshewa kiasi
cha kukosa amani, amelazimika kuvua taji ili awe huru.
“Habari
za jioni Watanzania wenzangu, kutokana na kuwa nimekuwa nikisemwa sana,
maneno mengi yasio na tija juu ya hili taji la U-Miss anzania
2014,,mpaka kupelekea nisiwe na amani na uhuru ndani ya nchi yangu
Tanzania, kwa roho safi nimeamua mwenyewe kujivua taji hilo na kuacha
wanayeona anastahili taji hili apewe ili niendelee na maisha yangu kwa
amani ,isiwe shida sana kwani sitegemei taji hili ili kuishi!!”
imeandikwa katika ukurasa huo.
Akizungumzia
uvumi huo, Lundenga alisema hakuna ukweli juu ya taarifa hiyo, na
kwamba kama lingekuwa na ukweli ni wazi kwamba Sitti angeiarifu kampuni
yake, inayoratibu kinyang’anyiro hicho kilichotimiza miaka 20 mwaka huu.
“Hakuna
taarifa iliyotufikia hadi sasa kuhusiana na taarifa hizo. Sitti anajua
anapaswa kufanya nini kama anaamua kulitema taji, ambapo anapaswa
kutuarifu sisi kabla ya kuripoti hilo mahali popote. Kwa kuwa hajafanya
hivyo, tunaamini hilo halipo na ndio tunamtambua kuwa mrembo wetu,”
alisema Lundenga.
Kwa
upande wa mama wa mrembo huyo, alisema ameshtushwa na taarifa za
mwanaye kujiuzulu na kusema si za kweli, kwani kama angepanga kufanya
hivyo asingefanya kwa kificho, badala yake angeitisha mkutao na
wanahabari: “Hawezi kujiuzulu kienyeji hivyo na hata mimi mama yake sina
taarifa hizo, hayo ni matumizi mabaya ya mitandao.”
credit: Mo dewji blog
No comments:
Post a Comment