Kisiga na Kiemba waliosimamishwa Simba |
Simba ambayo imekuwa na matokeo yasiyoridhisha tangu msimu uliopita imeelezwa iliwatimua kambini jijini Mbeya wachezaji hao wawili pamoja na Haruna Chanongo bila kuelezwa utovu wa nidhamu waliofanya.
Hata hivyo habari za ndani ya klabu zinasema kuwa watatu hao wametimuliwa kwa tuhuma za kuhusika na kuihujumu timu ili ipate matokeo mabovu katika mechi zake za ligi kuu.
Simba imecheza mechi 11 za ligi tangu msimu uliopita na huu wa sasa bila kupata ushindi ikiwa imeambulia sare tano mfululizo na kuzua maswali mengi kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.
Kisiga aliyerejeshwa Simba msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi kwa Simba akiwa na mabao mawili sawa na Emmanuel Okwi.
Aidha taarifa zaidi zinasema kuwa kocha msaidizi, Suleiman Matola na daktari wa timu wapo chini ya uchunguzi na benchi la ufundi kwa ujumla limepewa mechi tatu kuhakikisha wanashinda vinginevyo watatimuliwa.
Imekuwa ni desturi kwa viongozi wa soka nchini kila timu zao zikifanya vibaya badala ya kuangalia mambo ya msingi ikiwamo suala la ufundi hukimbilia kuwatuhumu wachezaji kuzifanyia hujuma bila ya kuwa na uthibitisho kitu kinachodaiwa ni kama kuwatoa KAFARA wachezaji KUFICHA UDHAIFU wao.
No comments:
Post a Comment